Serikali ya nchini Uganda imeanza kudhibiti mchakato wa kutoa hati za kusafiria za kidiplomasia./Picha: https://x.com/PassportsUganda

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uganda, Meja Jenerali Kahinda Otafiire amepiga marufuku utoaji wa pasipoti ya kidiplomasia kwa mtoto wa Balozi mdogo wa zamani wa Pakistan nchini Uganda.

Hatua hii inakuja katikati ya sintofahamu kuhusu ni kwa misingi gani Rugiirwa Katatumba, ambaye ni mtoto mfanyabiashara Bonney Katatumba Mwebesa anamiliki hati hiyo ya kidiplomasia wakati si mwanadiplomasia.

Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote uliotolewa kuhusiana na madai hayo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uganda, Meja Jenerali Kahinda Otafiire./Picha: 

“Nilifanya kazi Wizara ya Mambo ya Nje. Kwa mfano, mimi si Waziri wa Mambo ya Ndani kwa sasa, ni mwanadiplomasia wa zamani. Najua hivi vitu huwa vinafanyika. Hata watoto wa wanadiplomasia hawapewi hati za kidiplomasia baada ya kufikisha miaka 18, kwani wanabakia raia wa kawaida tu,” alisema Waziri huyo.

Kulingana na Otafiire, kama Mganda anafanya kazi nje ya nchi, basi atastahili kupata hati ya kidiplomasia.

“Nileteeni ushahidi kuwa anamiliki hati ya kidiplomasia ili nimnyang’anye,” alieleza.

Mapema wiki hii, Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani Arithea Nakiwala alisema kuwa nyaraka hiyo inaweza kuwa imetolewa kwa sababu mbalimbali.

“Inaweza kuwa Waziri ametoa hati hiyo kwa sababu maalumu kama vile ushawishi wa mtu huyo kibiashara na mchango wake kwa nchi,” alisema Nakiwala.

Raia wengi wa Uganda wamepeleka maombi ya kupatiwa pasipoti za kidiplomasia bila ya mafanikio yoyote.

Mwaka jana, mamlaka za nchi hiyo zilifuta maombi zaidi ya 288 ya hati za kidiplomasia kwa sababu zilishindwa kufikia vigezo na masharti yaliyowekwa.

TRT Afrika