Waziri wa Nchi Uganda anayehusika na Uhusiano wa Kimataifa, Okello Oryem amelaumu vikwanzo vya Marekani na Umoja wa Ulaya/ Picha:  Parliament Watch.

Waziri wa Nchi wa Uganda anayehusika na Uhusiano wa Kimataifa, Okello Oryem ametetea uamuzi wa Benki Kuu ya Uganda wa kuanza kununua dhahabu kutoka kwa wakulima wa ndani.

Amesema hatua hiyo inanuiwa kuikinga Uganda dhidi ya vitisho kutoka kwa Marekani iwapo taifa hilo litafungia hifadhi ya dhahabu ya Uganda bila mashaka.

“Sasa tuko katika mchakato wa kuchunguza, na maelezo yanaandaliwa kwa ajili ya Benki ya Uganda kuanza kununua dhahabu ili tuwe na akiba ya dhahabu katika nchi hii na siyo tu hifadhi ya dhahabu nje ya nchi," Oryem amesema,

"Tuna takriban Dola za Kimarekani Milioni 4 za akiba ya nje kulingana na Pato la Taifa. Tuna hatari ya Marekani kuweka vikwazo vya kufungia fedha hizo zote,” Oryem alisema.

Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje akiwasilisha Muswada wa Mfumo wa Bajeti wa 2025/2026.

Wabunge wengine walimtaka Waziri afafanue mazingira ambayo Uganda ilijiunga na BRICS na ni wajibu gani wa kifedha unakuja na uanachama huu.

"Miezi michache tu iliyopita, iliripotiwa sana kwamba Uganda ilijiunga na BRICS. Tunahitaji kuelewa jinsi Uganda ilivyojiuga na BRICS, na iwapo ina wajibu wowote wa kifedha kwa Uganda na jinsi tunavyochagua ushirikiano wetu wa kimataifa," Nkuyingi Muwada mbunge wa Kyadondo Mashariki aliuliza.

"Kwa sababu kwa upande mmoja tunasema, lazima tulipe ada za usajili. Lazima tuelewe, tunachaguaje mahali pa kujiandikisha kama nchi? Tulijiunga vipi na je, pia imeleta athari zozote za kifedha?" Mbunge alitaka kujua.

Oryem alielezea kuwa Uganda ililazimika kujiunga na muungano wa BRICS kutokana na mabadiliko ya mpangilio wa dunia ambapo Marekani na Umoja wa Ulaya zimekuwa zikiweka vikwazo kwa mataifa huku zikikiuka masuala hayo hayo.

"Marekani na Umoja wa Ulaya wakati wowote wanapoweka vikwazo, wanatarajia nchi nyengine zinatii vikwazo hivyo na usipofanya hivyo, utapata adhabu," alibainisha Waziri.

"Kwa sababu hiyo na matukio ya hivi karibuni, umegundua kuwa Marekani na Umoja wa Ulaya zimeanza kufungia mali za nchi katika mataifa yao bila maazimio ya Umoja wa Mataifa, jambo ambalo ni uvunjaji wa utaratibu wa kimataifa wa dunia. Uganda haiwezi kusimama tu na kuangalia mabadiliko haya na isiwe na sehemu ya kufanya mabadiliko haya, haitakuwa sawa," alisema Waziri Oryem.

Waziri aliwaambia wabunge kuwa kujiunga na BRICS haina athari zozote za kifedha.

"Jambo hili lilijadiliwa kwenye Baraza la Mawaziri, kisha Rais alitoa maagizo kwa Wizara ya Fedha kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuiandikia Sekretarieti ya BRICS kwamba Uganda ingependa kuwa ndani ya BRICS. Sijui kama inahitaji idhini ya Bunge au la, kwa sababu tulipokuwa wanachama wa mashirika hayo yote, sidhani kama ilihitaji idhini kutoka kwa Bunge,” Oryem alieleza.

TRT Afrika