Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza umetoa tahadhari ya usalama wake wa nchini humo, kufuatia vurugu zinazoendelea eneo hilo.
Katika tahadhari hiyo iliyochapishwa kwenye ukurasa wa X (zamani twitter), ofisi za ubalozi huo imewataka Watanzania waishio nchini Uingereza kuchukua tahadhari kufuatia vurugu zinazoendelea nchini humo.
Ubalozi huo, pia umesema kuwa uko tayari kuwasaidia raia wake endapo kutatokea hali ya dharura mpaka hali itakaporejea kawaida.
Vurugu hizo zimesababishwa na kusambaa kwa taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii kuhusu wahamiaji wa Kiislamu nchini humo, wanaodaiwa kuwauwa wasichana wadogo watatu.
Machafuko hayo yalitokea katika eneo la Southport, kaskazini mwa Uingereza, mapema wiki iliyopita.
Axel Rudakubana anatuhumiwa kuwauwa kwa kuwachoma kisu Alice Dasilva Aguiar, Bebe King na Elsie Dot Stancombe siku ya Julai 29, 2024.
Rudakubana anadaiwa kujeruhi watoto wengine wanane katika tukio hilo.