Kupata hati ya kusafiria, au pasipoti nchini Kenya imekuwa swala la sintofahamu.
Kuna watu ambao walioomba pasipoti rasmi na hata kulipia mwaka uliopita , lakini hadi sasa hawajapata.
Idara ya uhamiaji ilisema changamoto ilitokea kwa sababu mashine ya kuchapisha pasipoti ilikuwa imeharibika.
"Nimepokea taarifa za kuaminika kuwa changamoto kubwa ya pasipoti kutochapishwa ni ufisadi," Kithure Kindiki, waziri wa mambo ya ndani ameiambia kamati ya bunge.
"Mwezi Mei nilikubali tuna shida katika idara hii na ninataka kujitolea wazi kuwa tutasafisha Nyayo House kwa ufisadi na uhalifu mwingine."
Nyayo House ni jina la jumba ambapo idara ya uhamiaji ipo jijini Nairobi.
Mwezi Mei mwaka huu Waziri wa Mambo ya ndani Kindiki Kithure aliahidi kuwa pasipoti zingeanza kuchapishwa, lakini bado zaidi ya watu 40,000 hawajaona pasipoti zao.
"Ikinilazimu nitatangaza kuwa ofisi hizo za Nyayo House ni eneo za uhalifu"
Kindiki amewaambia wabunge wa kamati hiyo kuwa " itasimamisha shughuli, serikali itasimamisha ofisi hizo kwa ajili ya kufanya usafishaji usio na huruma na kuwaondoa kundi la maofisa wala rushwa wanaoendelea kuwakatisha tamaa waombaji huduma".
Wananchi katika mitandao ya kijamii wamekuwa wakijadili vile sasa ni lazima utoe rushwa ili upate pasipoti yako.
"Hatuelewi kwa nini mashine ya kuchapisha pasipoti za kidiplomasia iko lakini mashine hii hii haiwezi kuchapisha pasipoti za wananchi," mtu ammoja alisema katika mtandao wa X.
Mwingine naye akaongezea kuwa
"Ikiwa hauna dola 120 hadi dola 180 ya kuwapa rushwa maafisa katika idara hiyo, basi uta ngoja pasipoti yako mpaka usahau."