Tanzania na Somalia yaboresha ushirikiano katika sekta kadhaa

Tanzania na Somalia yaboresha ushirikiano katika sekta kadhaa

Ziara hii ya kihistoria inaashiria mwanzo mpya katika uhusiano wa Somalia na Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi amemkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, jijini Mogadisho 19 Disemba 2024. /Picha: MOFA Somalia

Na Mustafa Abdulkadir

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Ahmed Moalim Fiqi amemkaribisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mogadishu siku ya Jumatano 18 Disemba 2024.

Ziara hii ya kihistoria inaashiria mwanzo mpya katika uhusiano wa Somalia na Tanzania, huku mataifa yote mawili yakijiandaa kufanya makubaliano katika sekta mbalimbali yenye lengo la kuendeleza maslahi ya pande zote mbili na kukuza ushirikiano wa karibu.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta muhimu ikiwa ni pamoja na sekta ya ulinzi, utalii, afya na usafiri wa anga.

Kuhusu ziara hiyo, Waziri Kombo amesema, “ Namshukuru Mungu kwa kutuleta sisi pamoja hapa kwa misingi ya nia nzuri.”

Vile vile Waziri huyo amewapongeza marais wa Tanzania na Somalia kwa kuwezesha ziara hiyo.

Akisisitiza kuwa makubaliano muhimu kati ya nchi hizo yamejikita kwenye kuijenga tena Somalia hasa ushirikiano katika sekta ya ulinzi na usalama, akidokeza kwamba Somalia bila ya sekta hizo mbili muhimu haiwezi kukua kiuchumi.

Mwisho kabisa Waziri Kombo ametoa wito kwa raia wa Somalia kukuza lugha ya Kiswahili kama lugha ya Afrika Mashariki akisema ya kwamba Tanzania inajivunia kuwa nchi peke inayounganishwa na lugha ya Kiswahili.

TRT Afrika na mashirika ya habari