Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua eneo la maafa ya ajali ya kuporomoka kwa ghorofa katika soko la Kariakoo./Picha: @ikulumawasliano

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa idadi ya waathirika wa tukio la kuporomoka kwa jengo lenye ghorofa nne katika soko la Kariakoo, sasa imefikia 20.

Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo katika soko la Kariakoo, alipoenda kujionea athari za tukio hilo lililotokea Novemba 16, 2024, wakati akiwa nchini Brazil kuhudhuria Mkutano wa G20.

“Taarifa niliyopewa leo ni kwamba mpaka saa tatu asubuhi tumepoteza wenzetu 20 ambao serikali imeshirikiana na familia kuwasitiri wenzetu," alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Jitihada zetu kubwa katika tukio hili imekuwa kuwaokoa wenzetu walionasa katika jengo lile wakiwa hai lakini kama tunavyoambiwa jitihada haziondoshi kudra ya Mungu, pamoja na jitihada tulizofanya kuna wenzetu tumewapoteza.”

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwajulia hali na kuwapa pole majeruhi wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la biashara kwenye soko la Kariakoo, wakati alipowatembelea katika Hospitali ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam./Picha: @ikulumawasliano

Hata hivyo, Rais Samia aliapa kuchukua hatua kutekeleza maagizo ya tume iliyoundwa kukagua ubora wa majengo katika eneo la Kariakoo.

“Tutaweka wazi mapendekezo ya tume hiyo, na hatutosita kubomoa majengo ambayo hayatokuwa yametii vigezo vya viwango,” aliongeza.

Rais Samia, pia aligusia wazo la kutumia mapendekezo ya tume mbili zilizoundwa mwaka 2013, akisema kuwa mawazo yao yanaweza kusaidia katika utekelezaji wa maamuzi.

Mwaka 2006, Tanzania iliunda tume maalumu kuchunguza tukio la kuporomoka kwa jengo katika eneo la Keko jijini Dar es Salaam, tukio ambalo lilisababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi kadhaa.

Kiongozi huyo alisisitiza kuwa hatua stahiki zitachukuliwa baada ya ukaguzi kufanyika.

TRT Afrika