Tamasha la nyangumi nchini Madagascar linaendelea katika kisiwa cha Sainte-Marie kilichoko kaskazini-mashariki ambapo wanyama baharini wanajulikana kuzaliana.
Tamasha hilo, linalojulikana kwa jina la Zagnaharibe kwa lugha ya eneo hilo, linasherehekewa kila mwaka wakati nyangumi wanapojitokeza karibu na kisiwa hicho.
"Inasaidia kukuza ufahamu kuhusu nyangumi ambao huchagua maji ya joto ya Bahari ya Hindi kuzaliana na kulea watoto wao," kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Utalii.
Tamasha hilo, ambalo sasa linatimiza mwaka wake wa saba, lilianza Jumamosi na litakwenda hadi tarehe 23 Juni. Rais Andry Rajoelina alihudhuria sherehe rasmi ya ufunguzi.
Tamasha hilo ni tukio la kitamaduni na utalii - likiwaleta pamoja wenyeji na watalii kushuhudia nyangumi na kuadhimisha utamaduni na mila za eneo hilo.
Pia linasisitiza ulinzi wa nyangumi.
"Utalii ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni kwa kisiwa chetu. Hivyo, lazima tuhakikishe kuwa mahali ambapo watoto wanaishi linalindwa," alisema Ravonty Tena Luc, afisa wa eneo hilo.
Matukio mbalimbali ya michezo, utamaduni na utalii yamepangwa wakati wa tamasha hilo. Ziara za kuangalia nyangumi zimeandaliwa kwa ajili ya watalii kuwawezesha kuona nyangumi wakijitokeza majini.
Tangu kufunguliwa kwa mipaka ya anga baada ya mzozo wa afya wa Uviko-19, Kisiwa Kikubwa kimeitegemea utalii ili kufufua uchumi wake.Wizara ya utalii inatarajia watalii milioni moja kwa kipindi cha 2023 - 2028.