Wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali wamewatuhumu maafisa wa Taasisi ya Moyo ya Uganda kwa kurejesha zaidi ya dola laki 480 (Sh1.8Bn) kwa hazina ya jumla, ilhali awali walikuwa wamelalamikia kupunguzwa kwa bajeti kwa zaidi ya dola milioni1.3 (Shs 5Bn).
Kwa sababu ya kukatwa kwa bajeti, taasisi hiyo imelalamika kuwa baadhi ya wagonjwa walifariki na wengine kuachwa kutokana na kukosa fedha za matibabu.
Dk. John Omagino, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Uganda aliwaambia wabunge kuwa zaidi ya dola laki 480 zilizorejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali mwishoni mwa 2022/23 ni fedha zilizokusudiwa katika ujenzi wa majengo mapya ya Taasisi hiyo yaliyopo Naguru, jijini Kampala.
Lakini idhini ya mradi huo ilicheleweshwa, na kusababisha fedha hizo kurejeshwa kwenye hazina ya Serikali. Uongozi wa taasisi hiyo unasema fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya sherehe za kuanzisha msingi, mawasiliano kwa umma, umeme, usambazaji wa maji na njia za maji taka.
Omangino pia aliwafahamisha wabunge kwamba huduma zinazotolewa katika Taasisi ya Moyo ya Uganda zina ruzuku ya juu na kupunguzwa kwa bajeti yoyote kunaathiri wagonjwa.
"Huduma za Taasisi ya Moyo ya Uganda zina ruzuku kubwa, zinalipa robo ya bei ya soko kwa hivyo suala ni, pesa inaingia kwenye huduma nyengine zinazounga mkono mfumo na mara unapokata, usambazaji wa vitu hivi vyote, uwezo wako wa kupata vitu hivyo vingine."
Alisema Taasisi ya Moyo ya Uganda inatoza dola za Marekani 5000 (Sh 18,864,427) kwa ajili ya upasuaji wa moyo lakini wengi wa wagonjwa hao hawana uwezo wa kumudu fedha hizo hivyo, wengine huishia kulipa 50% au baadhi yao hulipa sifuri kwa huduma hizo.
Lakini mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali katika bunge ya Uganda, Muwanga Kivumbi alimtaka Dk. Omangino kueleza kwa nini taasisi hiyo haikuomba ruhusa kwa Wizara ya Fedha kuweka fedha walizorudisha kwa matumizi ya matibabu.
“Hizi fedha unapokuwa na dharura unaweza kuomba. uhamishaji upya. Je, ulijaribu kuiomba ikakataliwa? Inasikitisha sana kwamba uliruhusu pesa kurudi na huku unalalamika kupunguzwa kwa bajeti. Kwa hivyo, upunguzaji wa bajeti ulikushtua, hukuweza hata kutumia kidogo ulichonacho,” Kivumbi alisema katika kikao hicho cha bunge.
Taasisi ya Moyo ya Uganda ipo chini ya Wizara ya Afya ya Uganda na inahudumia zaidi ya wagonjwa 20,000 kila mwaka.
Ilianza kufanya upasuaji wa moyo wazi mwaka 2007 na hadi sasa inaripotiwa kuwa zaidi ya upasuaji wa moyo 7000 umefanywa.