Mapigano ya zaidi ya wiki mbili kati ya jeshi la Sudan na kundi la wanamgambo la RFS katika mji mkubwa wa jimbo la Darfur, yamesababisha vifo vya takriban watu 123, shirika la misaada la kimataifa lilisema Jumapili.
Mapigano huko el-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, pia yalijeruhi zaidi ya watu 930 katika kipindi hicho, madaktari wasio na mipaka walisema.
"Hii ni ishara ya kukithiri kwa mapigano," kundi hilo lilisema.
"Tunaziomba pande zinazozozana kufanya zaidi kulinda raia."
Zaidi ya watu 14,000 wameuawa nchini Sudan
Mapigano kati ya wanajeshi na wanamgambo wa RFS yameongezeka mapema mwezi huu katika jiji hilo, na kuwalazimu maelfu ya watu kukimbia makazi yao, kulingana na Umoja wa Mataifa.
El-Fasher imekuwa kitovu cha mzozo kati ya jeshi na RSF. Mji huo ndio ngome ya mwisho ambayo ingali inashikiliwa na wanajeshi katika eneo kubwa la Darfur.
Mzozo wa Sudan ulianza mwezi Aprili mwaka jana, wakati mvutano uliokuwa ukiongezeka kati ya viongozi wa jeshi na RSF ulipozuka, na kusababisha mapigano ya wazi katika mji mkuu, Khartoum, na kwingineko nchini humo.
Mzozo huo umeua zaidi ya watu 14,000 na kujeruhi maelfu zaidi, huku kukiwa na ripoti za kuenea kwa unyanyasaji wa kingono na ukatili mwingine, ambao mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.
Njaa
Vita hivi vimesababisha njaa kwa idadi kubwa ya wakazi wa Sudan. Shirika la Umoja wa Mataifa la chakula lilionya pande zinazopigana mapema mwezi huu, kwamba kuna hatari kubwa ya kuenea kwa njaa na vifo huko Darfur na kwingineko nchini Sudan ikiwa hawataruhusu msaada wa kibinadamu katika eneo hilo kubwa la magharibi.
RSF imeunda vikosi katika miezi ya hivi karibuni kutaka kuteka udhibiti wa el-Fasher. RSF iliuzingira mji huo na kuanzisha mashambulizi makubwa katika maeneo yake ya kusini na mashariki mapema mwezi huu.
Mapigano hayo yalianza tena siku ya Alhamisi katika kambi ya Abu Shouk ya watu waliokimbia makazi yao katika kitongoji cha Salam, kaskazini na kusini-magharibi mwa mji huo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa liliripoti.
Siku ya Jumamosi, bomu lililenga nyumba ya mfanyakazi wa shirika la Madaktari Wasio na Mipaka karibu na soko kuu la jiji, na kumuua mfanyakazi huyo, shirika la kutoa misaada lilisema.