Kamanda wa kijeshi wa kikundi cha Rapid Support Forces, Mohamed Hamdan Dagalo, alikutana na rais Willima Ruto jijini Nairobi tarehe 3 Januari mwaka 2024.  Picha. Ikulu Kenya

Sudan imemrudisha nyumbani balozi wake kutoka Nairobi kama ishara ya kupinga kitendo cha Rais wa Kenya William Ruto kuandaa mazungumzo na kamanda wa kijeshi wa kikundi cha Rapid Support Forces, Mohamed Hamdan Dagalo, kaimu waziri wake wa mambo ya nje amesema.

Mkutano huo ulikuwa tarehe tatu mwezi Januari mwaka huu, jijini Nairobi,

Dagalo, ambaye vikosi vyake vimekuwa vitani na jeshi la serikali ya Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan tangu Aprili, amekuwa akizuru miji mikuu ya Afrika katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi.

Tayari alitembelea Uganda, Ethiopia na Djibouti pamoja na Kenya, na kwa sasa yuko Afrika Kusini,jambo amabalo halimfurahishi jenerali Al Burhan.

Katika taarifa iliyotolewa na shirika rasmi la habari la SUNA la Sudan, siku ya Alhamisi, kaimu waziri wa mambo ya nje wa Sudan Ali al-Sadiq alisema balozi huyo ameitwa "kwa mashauriano ya kupinga mapokezi rasmi yaliyoandaliwa na serikali ya Kenya..."

Vita vya mauti

Alisema mashauriano hayo "yatashughulikia uwezekano wote wa matokeo ya uhusiano wa Sudan na Kenya."

Uhusiano kati ya Burhan na serikali ya Kenya umedorora kwa miezi kadhaa, huku Nairobi ikijaribu kuweka njia za mawasiliano wazi na Dagalo ili iweze kupatanisha katika mzozo huo.

Vita vya Sudan vimewauwa zaidi ya watu 12,190, kulingana na makadirio ya kihafidhina kutoka kwa Mradi wa 'Armed Conflict Location and Event Data' Project. Zaidi ya watu milioni saba wamelazimika kukimbia makazi yao, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.

Juhudi za upatanishi zimesimama kwa kiasi kikubwa.

TRT Afrika