Tangu Aprili 2023 vita vinaendelea kati ya jeshi la serikali ya Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces./Picha: Wengine

Kamati ya Umoja wa Mataifa ya kukagua kiwango cha njaa imethibitisha pasipo na shaka, kiwango kikubwa cha njaa katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam, iliyo karibu na mji wa El Fasher, ndani ya jimbo la Darfur.

Vita vilivyodumu kwa miezi 15 ndani ya nchi hiyo, vimesababisha madhara kadhaa yakiwemo uhamaji wa watu na njaa kubwa, inayowakumba watu wengi waishio maeneo ya Darfur Kaskazini mwa Sudan.

"Tunahitaji kwa haraka upanuzi mkubwa wa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu ili tuweze kukomesha njaa katika eneo la Darfur Kaskazini na kukomesha kuenea kote Sudan," Mkurugenzi Mtendaji wa WFP Cindy McCain alisema katika taarifa.

Tangu Aprili 2023, nchi hiyo imeshuhudia vita kati ya Jeshi la serikali ya Sudan na kikundi cha Rapid Support Forces(RSF).

" Pande zinazopigana lazima ziondoe vikwazo vyote na kufungua njia mpya za usambazaji mipakani, na katika maeneo ya migogoro, ili mashirika ya misaada yaweze kufika kwa jamii zilizo katika hali mbaya na chakula na misaada mingine ya kibinadamu inayohitajika," aliongeza McCain.

UN imesema kuwa tangazo la njaa katika eneo hilo linathibitisha hofu ya jumuiya ya kibinadamu na linafuata uchambuzi wa mwezi Juni unaoonyesha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa usalama wa chakula na lishe, huku watu 755,000 wakikabiliwa na hali mbaya.

" Kama misaada ya dharura haiwezi kuwasilishwa kwa jamii zilizokwama katika maeneo yenye migogoro kama vile Darfur, Khartoum, Kordofan na Al Jazirah. Hali bado ni mbaya nchini kote, huku takriban watoto 730,000 wakitarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu," imeongeza UN.

Pata habari zaidi kupitia Whatsapp channels

.

TRT Afrika