Salva Kiir na Riek Machar wametawala siasa za Sudan Kusini tangu uhuru wake 2011/ Picha: Nyingine

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ameahidi kuwa uchaguzi uliocheleweshwa kufanyika mwaka ujao utaendelea kama ilivyopangwa.

"Tumejitolea kutekeleza sura za mkataba wa amani na uchaguzi utafanyika mwaka wa 2024," alisema Jumanne.

Salva Kiir amesema atawania kiti cha urais.

Taifa hilo changa zaidi duniani linajitahidi bado haijajikwamua kutoka kwa mizozo tofauti ambazo zilianza 2013 baada ya mvutano kati ya makamu wa rais wa sasa Riek Machar na Rais Salva Kiir .

Kipindi cha mpito ulifaa kukwisha na uchaguzi kufanyika mnamo Februari 2023, lakini serikali hadi sasa imeshindwa kufikia vifungu muhimu vya makubaliano, ikiwa ni pamoja na kuandaa katiba.

"Ninakaribisha uamuzi wenu wa kuniteua kugombea urais mwaka wa 2024," Kiir aliwaambia wafuasi wa chama chake tawala cha Sudan People's Liberation Movement (SPLM) siku ya Jumanne, wakati wa hafla katika eneo la Greater Bahr El Ghazal .

Ilikuwa sherehe ya kuidhinishwa kwake na chama.

Tarehe kuhairishwa

Mnamo Agosti, viongozi Rais Salva Kiir na Makamu wake Riek Machar, waliongeza serikali yao ya mpito kwa miaka miwili zaidi ya muda uliokubaliwa wakitaja haja ya kushughulikia changamoto zilizokwamisha utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Kiir alisema kuwa changamoto hizo zitashughulikiwa "kabla ya uchaguzi" uliopangwa kufanyika Desemba mwaka ujao.

Hakuna mwanasiasa mwingine aliyetangaza kugombea lakini mpinzani wake wa kihistoria Riek Machar anatarajiwa kugombea.

Shinikizo la Umoja wa Mataifa

Ikiwa kati ya nchi maskini zaidi duniani licha ya hifadhi kubwa ya mafuta, Sudan Kusini imetumia takriban nusu ya maisha yake kama taifa katika vita.

Takriban watu 400,000 walikufa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano, tangu 2013 kabla ya Kiir na Machar kutia saini mkataba wa amani mwaka 2018 na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukiukosoa mara kwa mara uongozi wa Sudan Kusini kwa jukumu lake la kuchochea ghasia, kukandamiza uhuru wa kisiasa na kupora hazina za umma.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini Nicholas Haysom alionya mwezi Machi nchi hiyo inakabiliwa na mwaka wa "kujiunda au kujimaliza" mwaka 2023, na viongozi wake lazima watekeleze makubaliano ya amani ya kufanya uchaguzi "jumuishi na wa kuaminika" mwaka ujao.

Haysom alisisitiza Juba "imesema wazi kwamba hakutakuwa na nyongeza za muda" wa uchaguzi mwishoni mwa 2024.

TRT Afrika na mashirika ya habari