Mwanasiasa Kizza Besigye na mshitakiwa mwenzake, Obeid Lutale Kamulegeya watasalia rumande katika Magereza ya Luzira hadi Disemba 2, 2024/ Photo: Reuters

Spika wa Bunge la Uganda ameitaka serikali ya nchi hiyo kuleta ripoti kamili wiki ijayo, kueleza mazingira ambayo aliyekuwa mgombea urais, Kizza Besigye na mshitakiwa mwenzake, Obeid Lutale Kamulegeya walichukuliwa kutoka nchini Kenya kinyume cha sheria, na kufikishwa mahakamani na kufikishwa katika Mahakama ya Kijeshi.

Maagizo yake yalifuatia kauli iliyotolewa na Ssemujju Nganda mbunge wa Manispaa ya Kira, ambaye alipinga namna Besigye, mmoja wa wahamasishaji wa chama kipya cha siasa kilichoanzishwa, People's Front for Freedom (PFF) alivyotekwa nyara kutoka Kenya.

Besigye alikuwa amekwenda kuhudhuria mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kitabu cha aliyekuwa Waziri wa Sheria Kenya Martha Karua.

Mbunge huyo amesema kuna haja ya serikali kuelezea zaidi kwani taarifa za Besigye kutekwa nyara zilizuka Novemba 19, 2024 baada ya siku tatu ya tukio lake la kutoweka.

Hata hivyo, mbunge mwengine Hamson Obua aliutaka uongozi Bungeni kutoharakisha kulaani kutekwa kwa Besigye kutoka Kenya akisema kesi ya Besigye itaungwa mkono na ushahidi ulioletwa na upande wa mashtaka na matokeo yake yatajulikana hadharani.

"Ninachoweza kuthibitisha kwa niaba ya Serikali, ni kile ambacho kiko mbele ya umma kwamba Besigye alikamatwa, akafikishwa mahakamani, akashtakiwa na kurudishwa katika Gereza la Luzira," Obua aliliambia bunge.

Asuman Basalirwa mbunge wa Manispaa ya Bugiri alikataa majaribio ya Serikali ya kujificha nyuma ya kanuni ya uasi na kuepuka kueleza uvunjaji sheria uliofanyika wakati wa kutekwa nyara kwa Besigye na Lutale kutoka Kenya kwenda Uganda.

“Hata hivyo, kuna masuala mawili ambayo Serikali inapaswa kuyatolea ufafanuzi. Hilo linahusiana na uhusiano wetu na Kenya hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba tuna mkataba wa kurejesha wanaokamatwa kwa nchi hiyo. Wananchi wa Uganda wako salama kiasi gani?" Basalirwa aliuliza.

Besigye alishtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama na kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Wawili hao watasalia rumande katika Magereza ya Luzira hadi Disemba 2, 2024.

TRT Afrika