Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among ameelezea kutoridhishwa kwake na mahudhurio duni ya wabunge wakati wa Kikao Maalumu kilichoitishwa kumuenzi mbunge aliyefariki Januri 9, 2025, Muhammad Ssegirinya.
Hii ilikuwa baada ya benchi la mbele lililotengwa kukaliwa na Baraza la Mawaziri na wabunge wa chama tawala cha NRM kusalia bila watu.
"Na inapotokea jambo kama hili, sote tunapaswa kuwa hapa, kumpa mwenzetu heshima, hakuna siasa katika mambo haya. Kamwe tusiwe na siasa wakati tumepoteza wa kwetu kwa sababu ni mimi leo kesho ni mtu mwingine," alisema Spika akiwa Bungeni wakati wa kuaga mwili wa marehemu.
Tofauti na wakati mwengine ambapo kwa kawaida Waziri Mkuu Robinah Nabbanja au maafisa wa serikali huongoza upande wa Serikali katika kutoa heshima wakati wa vikao maalum, safari hii, Serikali ilionekana kususia shughuli hiyo.
Baada ya muda Naibu Waziri Mkuu wa Tatu wa serikali, Rukia Nakadama alikuja bungeni.
Aliomba radhi kwa niaba ya Mawaziri zaidi ya 80 kwa kutelekeza mwili wa Ssegirinya, akihusisha kitendo cha Serikali kutopata mawasiliano wakati kikao Maalum kilifanyika.
Hata hivyo, Spika wa bunge alikataa hoja hiyo akisema haikuwa kweli.
“Sitaki kuamini habari hizo za upotoshaji kwa sababu kama ni kweli mimi mwenyewe ningekubali kuwajibika. Maelezo ya bunge yako wazi kabisa na nilipoahirisha Bunge jana, nilisema, tunaahirisha hadi saa tatu za asubuhi, ” Spika alisema.
Ssegirinya alikuwa Mbunge kutoka upinzani, mwanachama wa NUP, chama kinachoongozwa na Robert Kgyagulanyi, maarufu kama 'Bobi Wine' kwa jina lake la usanii.
Ssegirinya kwanza alipata kujulikana na wananchi kupitia ushiriki wake katika vipindi vya mazungumzo kupitia Redio ya Kampala.
Siku chache tu baada ya kuapishwa mbunge 2021, Ssegirinya alikamatwa na kushikiliwa kwa takriban siku 500.
"Akiwa gerezani, Ssegirinya aliugua na hali yake iliendelea kuwa mbaya siku hadi siku, alinyimwa dhamana kila wakati, ingawa hali yake ilikuwa ya wasiwasi," Kiongozi wa upinzani bungeni Joel Ssenyonyi aliliambia Bunge.
"Hata madaktari wa Serikali walipopendekeza apatiwe matibabu maalumu ambayo yalimpa dhamana, hakimu bado alimpeleka gerezani ambako hali yake iliendelea kuwa mbaya kila kukicha. Mawakili wake walitoa ombi na kuwasilisha mahakamani kumbukumbu za matibabu zilizosainiwa na madaktari wa Serikali, wakisema mtu huyu aachiliwe kwa dhamana ili aende kupata matibabu maalum, hakimu alisema 'Hapana, rudi gerezani,'" Joel amesema.