Shimaa Tarek mbali na kazi ya ukalimani, pia ni mwalimu wa lugha ya Kiswahili nchini Misri. /Picha Shimaa

Na Edward Qorro

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Ni ukweli usiopingika kuwa lugha ya Kiswahili imefikia mamilioni ya wazungumzaji Afrika na ulimwenguni kwa ujumla.

Kati ya hao, yupo Shimaa Tarek, mzaliwa wa nchini Misri ambaye anashangaza watu kutokana na uhodari wake wa kuzungumza Kiswahili.

“Ni vyema uwe mwanafunzi mzuri na msikivu unapokuwa kwenye safari ya kujifunza lugha mpya, nadhani hiyo ndiyo siri kubwa kwangu ingawa sijawahi kutembelea nchi zenye kuzungumza lugha hiyo,"

Shimaa Tarek, mwalimu wa lugha ya Kiswahili nchini Misri

Tofauti na watu wengi, Shimaa, ambaye ana umri wa miaka 25, alianza kujifunza lugha adhimu ya Kiswahili akiwa na miaka nane tu.

Shimaa akiwa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri, Dkt. Emmanuel Nchimbi./Picha: Shimaa

“Nimezaliwa nchini Misri na nilianza kujifunza Kiswahili nikiwa binti mdogo tu,” anasema Shimaa katika mahojiano yake na TRT Afrika.

Kulingana na Shimaa mwenyewe, alianza kusikia lugha hiyo ikizungumzwa Afrika Mashariki ndipo alipovutiwa na kuamua kujifunza lugha hiyo.

“Nilivutiwa na lugha hiyo kwa sababu ya urahisi wake, hasa kutokana na kuwa ina maneno mengi kutoka lugha ya Kiarabu, jambo hili lilinifanya niweze kuielewa kwa haraka,” anaelezea.

Shimaa akiwa kwenye moja ya mijadala ya Kiswahili./Picha: Shimaa

Shimaa anasema ilimchukua miaka minne kuanza kuzungumza kwa ufasaha lugha ya Kiswahili.

Kwa sasa, imekuwa ni jambo la kawaida sana kumuona Shimaa akizungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha zaidi, hasa anapokuwa katikati ya wajuzi wa lugha hiyo.

Mbunge wa Wilaya ya Lubero, nchini DRC, Katembo Thadee, aliwafurahisha wajumbe wenzake alipohutubia bunge la nchi hiyo...

Posted by TRT Afrika Swahili on Sunday, October 20, 2024

Kama anavyosema mwenyewe, lugha ya Kiswahili imekuwa sehemu ya maisha yake hasa anapokuwa katikati ya wageni kutoka mataifa mbalimbali, japo hajawahi kutembelea nchi zinazozungumza lugha hiyo.

“Ni vyema uwe mwanafunzi mzuri na msikivu unapokuwa kwenye safari ya kujifunza lugha mpya, nadhani hiyo ndiyo siri kubwa kwangu ingawa sijawahi kutembelea nchi zenye kuzungumza lugha hiyo," anasema.

Kivutio mbele za watu

Uwezo wake wa kuzungumza lugha hiyo kwa ufasaha umemfanya Shimaa kuwa mfasiri wa lugha hiyo huku watu wengi wanaovutiwa naye wakitaka awe mkufunzi wa lugha hiyo pia.

Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limetambua mchango wa Shimaa katika kukuza Kiswahili./Picha: Shimaa

Ukuaji wa Kiswahili nchini Misri

Shimaa anaamini kuwa lugha ya Kiswahili imeanza kuenea vizuri nchini Misri kuliko wakati mwingine wowote, huku watu wengi wakionesha nia ya dhati ya kujifunza lugha hiyo.

Kulingana na Shimaa, kwa sasa, lugha ya Kiswahili imeanzwa kufundishwa kwenye vyuo vikuu vinne nchini Misri, ambavyo ni Ain Shams, Al-Azhar, Cairo na Aswan.

Fursa zitokanazo na Kiswahili

Kama ilivyo kwa lugha nyengine, Kiswahili kina fursa lukuki kwa wazungumzaji wake.

“Kwanza, wanaosoma lugha ya Kiswahili watapata faida ya kufahamu utamaduni wa Afrika Mashariki na historia yake na vile vile kuweza kutembelea eneo hilo ambalo nchi chimbuko la lugha hiyo,” Shimaa anasema.

Maadhimisho yanafanyika sehemu mbali mbali ya siku ya Kiswahili Duniani. Jumuiya ya Afrika Mashariki imewakaribisha watu...

Posted by TRT Afrika Swahili on Sunday, July 7, 2024

Si hayo tu, wazungumzaji wa lugha hiyo pia wana fursa ya kupata ajira kupitia lugha ya Kiswahili, kama ilivyo kwa Shimaa mwenyewe, ambaye kwa sasa ni mhadhiri wa lugha ya Kiswahili nchini Misri.

TRT Afrika