Rais William Ruto ametia saini Mswada wa Tume ya Uchaguzi, IEBC ya 2024 ambayo ilifanyiwa marekebisho.
Mswada huo uliopitishwa na Bunge unatokana na mapendekezo ya ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Majadiliano (NADCO).
"Kuidhinishwa kwa mswada wa IEBC leo ni alama muhimu katika uhalisia wa mojawapo ya mapendekezo na kushuhudia uwezo wa nchi yetu kushughulikia masuala magumu na wakati mwengine tata ambayo yanaweza kudhoofisha taifa letu kama uwajibikaji wa uwiano wa kitaifa na usalama ikiwa tutaacha bila kushughulikiwa," Rais William Ruto amesema wakati wa utiaji saini sheria hiyo jijini Nairobi.
Rais Ruto amesema kutiwa saini kwa muswada huu kunafungua njia kwa jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC .
"IEBC yabadilisha demokrasia yetu kusimamia uchaguzi katika viwango tofauti na kwa ujumla kuhakikisha kwamba mzunguko wetu wa uchaguzi unasimamiwa kwa uwazi na kusimamiwa kwa njia sahihi isiyoegemea upande wowote na namna ya kuwajibika."
Kusaini muswada wa kuunda upya tume ya uchaguzi ilikuwa kati ya matakwa ambayo vijana waliwasilisha kwa rais Ruto alipofanya majadiliano nao Julai 5, 2024 katika mtandao wa X .
"Nataka kusisitiza kwamba sasa tuangalie jambo zima kwa mfano sasa tumeanzisha mchakato wa kuteua makamishna tuliweke wazi kabisa - labda rais na waziri mkuu wa zamani Raila, tunaweza kukubaliana kwa mfano nani anakuwa mwenyekiti wa IEBC mpya. Hilo suala la kujadiliana ni muhimu," Kalonzo Musyoka, makamu wa rais wa zamani alielezea.
"Wakati nchi iko njia panda tunaweza ili kuanza kuifikisha nchi kwenye hali ya utulivu. Je, bwana rais unaweza kumuamuru inspekta jenerali wa polisi ikiwa hatajiuzulu anaweza kuwaondoa polisi mitaani na jeshi linaweza kuondoka mitaa yetu na kurudi kwenye kambi zao?" Kalonzo alimpa Rais Ruto changamoto.
Tuko kwenye hatua muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Nchi imesonga mbele na historia yetu ya miaka 61 tunahitaji sasa ushirikiano mpana zaidi ili watu wapate fursa ya kutapika kila kilichomo vifuani mwao ili kutafuta njia ya kusonga mbele," Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio, Raila Odinga alisema.
Sheria mpya ya uchaguzi ina nini?
Bunge la Kenya limeelezea mabadiliko katika sheria ya tume ya uchaguzi ambayo ina nia ya kuboresha mfumo wa uendeshaji wa IEBC.
Ili kuimarisha ujumuishaji na uwazi wa jopo la uteuzi wa IEBC, Muswada ulipendekeza kupanua jopo kutoka kwa wanachama saba hadi tisa na kurekebisha mchakato wa uteuzi.
"Inaamuru Tume ya Utumishi wa Bunge kufadhili shughuli za jopo, kuhakikisha rasilimali za kutosha kwa michakato kamili na isiyo na upendeleo ya uteuzi. Jopo hilo litakuwa na siku 90 kukamilisha kazi yake ya kuajiri, na uwezekano wa kuongezwa kwa kutegemea idhini ya bunge," maelezo kutoka tovuti ya Bunge imesema.
Muswada huu pia ulilenga kupanua vigezo vya uteuzi wa Tume kwa kuingiza utaalamu wa teknolojia ya habari na uhasibu. Mseto huu wa ujuzi unatarajiwa kuimarisha ufanisi wa Tume.
Sheria mpya imeondoa masharti yanayomruhusu makamu mwenyekiti au mjumbe yeyote kukaimu nafasi ya uenyekiti iwapo kuna nafasi. Hatua hii inakusudiwa kuunganisha uongozi na kudumisha mienendo iliyo wazi ya uwajibikaji ndani ya tume.
Muswada unapendekeza kupunguza muda wa Katibu wa Tume kutoka miaka mitano hadi miaka minne. Marekebisho haya yanalenga kuoanisha umiliki na mzunguko mpana wa utawala na kukuza mwendelezo.
Kulingana na sheria mpya IEBC itahitajika kuchapisha ripoti ya kina ndani ya miezi 18 baada ya uchaguzi, ambayo itawasilishwa Bungeni. Kifungu hiki kimeundwa ili kuhakikisha uboreshaji unaoendelea katika michakato ya uchaguzi.
Muswada uliainisha taratibu mpya za kazi inayohitaji ripoti kuzingatiwa na Bunge pekee.
Muswada huo ulijumuisha masharti ya mpito ya kusimamia uvunjwaji na uundaji upya wa jopo la uteuzi, kuhakikisha uendelevu katika majukumu ya Tume.