Ethiopia inayoshika nafasi ya 7 duniani kwa mauzo ya kahawa na inazalisha wastani wa tani 400,000 za kahawa kila mwaka / Picha: AFP

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Wewe unapokunywa kahawa yako, unaweka tu kwenye kikombo chochote na kuinywa, lakini nchini Ethiopia, kunywa kahawa ni jambo linalopewa heshima na thamani katika jamii hiyo.

Nchini Ethiopia, kahawa si mmea tu wa kawaida, mbali na kuwa chanzo cha mapato, kahawa ni nguzo muhimu ya utamaduni wa watu wa nchi hiyo iliyo katika pembe ya Afrika.

Ethiopia inayoshika nafasi ya 7 duniani kwa mauzo ya kahawa na inazalisha wastani wa tani 400,000 za kahawa kila mwaka.

Kunywa kahawa nchini humo ni sherehe ya kipekee inayoifuata mtindo maalumu / picha AFP 

Na licha ya kuuza zaidi ya tani 250,000 kila mwaka kwa nchi za nje, hii ni kati ya nchi ambapo wananchi wake wanakunywa sana kahawa wanayozalisha.

.Kunywa kahawa nchini humo ni sherehe ya kipekee inayoifuata mtindo maalumu

Na hii hufanyika kote nchini humo.

Tuchukue mfano wa nyumba za kawaida tu.

Baada ya mlo, mama mwenye nyumba au wasichana huvalia nguo za kitamaduni.

Nyasi hutandazwa sakafuni. Buni zinakaangwa mbele ya watu na mvuke wake hupuliza waliokaribu.

Nyasi hutandazwa sakafuni kama mpangilio muhimu katika sherehe ya kutengeneza kahawa/ Picha : AFP

Maji yanaweka katika birika inayoitwa ‘djebena,' huku kahawa inasagwa. Poda ya kahawa inawekwa katika maji yanayochemka, na kuwachwa kuchemka pole pole kwa muda.

Baada ya hapo, kahawa sasa inamwagwa katika vijikombe vidogo vidogo ambavyo huwa vimepangwa katika meza ndogo maalumu kwa sherehe. Chai inamwagwa kwa juu.

Watu wengine wanapenda kuongeza sukari, wengine huweka chumvi, na katika maeneo mengine ya Ethiopia watu huongeza mafuta ya siagi.

Baadae, maji huwekwa tena kwenye birika, na inanywiwa mara ya pili na ya tatu. Wageni ndio wanaoanza kuandaliwa, na ni watu wanywe mara mbili au tatu.

Buni zinakaangwa mbele ya watu na mvuke wake hupuliza waliokaribu/ Picha: AP

Hii ni sherehe ya kahawa kwa kila familia nchini Ethiopia. Awamu wa kwanza inaitwa Abol, ya pili inaitwa Tona na ya tatu inaitwa baraka.

Sherehe hii ya kahawa ni zaidi tu ya kunywa kahawa.

Watu wanapokunywa kahawa ni ishara ya umoja au urafiki kwani wanapata muda wa kujadiliana masuala muhimu.

Ni wakati wa kutatua mizozo na kufanya mipango hata ya maendeleo. Na hii ni sherehe ambayo inapitishwa kwa kizazi kimoja hadi chengine, haijalishi ni ndani ya nchi au nje.

TRT Afrika