Mamlaka ya afya ya Sudan imesema watu 17 wakiwemo watoto watano waliuawa katika shambulio la anga kusini mwa Khartoum Jumamosi.
"Wilaya ya Yarmouk ililengwa na mashambulizi ya anga na makadirio ya mapema yanaonyesha mauaji ya watu 17 na watoto watano miongoni mwao. Pia kumekuwa na uharibifu wa nyumba 25," idara ya afya ya mji mkuu wa Sudan ilisema katika ukurasa wake wa Facebook.
Mapigano yamepamba moto nchini Sudan tangu Aprili kati ya mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake wa zamani Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF).
Inakadiriwa kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,000.
Shirika la Kimataifa la Uhamiaji linasema kuwa takriban watu milioni 2.2 wamekimbia makazi yao, wakiwemo 528,000 ambao wamekimbilia nchi jirani.
Wakati huo huo madaktari Jumamosi walisema wameshindwa kumudu mamia ya majeruhi wanaokimbia jimbo la Darfur nchini Sudan, ambalo limekuwa kitovu cha wasiwasi wa kimataifa zaidi ya miezi miwili ya vita nchini humo.
Takriban watu 1,100 wameuawa katika eneo la El Geneina, Darfur Magharibi, kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Waliouawa ni pamoja na gavana wa Darfur Magharibi Khamis Abdullah Abakar, aliyeuawa baada ya kuwakosoa wanamgambo hao katika mahojiano ya televisheni Jumatano.
RSF ilikataa kuwajibika.
"Hali ni mbaya sana kusema ukweli, lakini kila mmoja anafanya kila awezalo kukabiliana nayo", alisema Seybou Diarra, mratibu wa mradi wa shirika la misaada la madaktari wasio na mipaka (MSF) katika eneo la Adre, Chad.