Maiti kumi zilipatikana Ijumaa katika kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya huku maafisa wakiendelea na uchunguzi wa namna waumini wa kanisa hilo walivyo hadaiwa na mhubiri Paul Mackenzie.
Idadi kamili ya vifo katika kanisa hilo imefikia 336, serikali ya Kenya imesema.
Waumini hao, kwa mujibu wa uchunguzi wa serikali, waliagizwa na Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko mbaroni, kuwa wajinyime kula na kunywa hadi kufa, katika matayarisho ya kukutana na Yesu.
Mamia ya maiti zimekutwa katika makaburi ya pamoja katika msitu mkubwa wa Shakahola mjini Malindi.
Ufukuzi umesitishwa kwa muda
Serikali imetangaza kusitisha kwa muda awamu ya tatu ya kuchimbua makaburi hayo ili kutoa nafasi ya kufanyiwa maiti uchunguzi kujua chanzo cha kifo. Kwa mujibu wa kamishna wa polisi wa mkoa wa pwani Rhoda Onyancha, maiti 94 zilipatikana katika wiki mbili zilizopita.
Idadi ya watu waliookolewa kutoka itikadi hiyo ya mauaji ya shakahola imefikia 95, japo hakuna manusura waliopatikana katika awamu hii ya tatu.
Zaidi ya wafuasi 600 wa kanisa hilo wanadaiwa kutoweka hadi sasa kwa mujibu wa kumbukumbu za serikali.
Serikali inasema itawafungulia washukiwa mashtaka ya mauaji ya halaiki, usaidizi wa kujiua, na ukatili dhidi ya watoto, miongoni mwa mashtaka menigne.