Henry Musasizi, Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Fedha Uganda amekiri kwamba akaunti za Benki Kuu zilidukuliwa/  Picha : Parlaiment Watch on X 

Serikali Ya Uganda imekiri kwamba akaunti za Benki Kuu ya nchi hiyo zilidukuliwa na kuibiwa, ingawa ilikanusha kwamba kiasi kilichoibiwa ni dola milioni 17 au shilingi bilioni 62 kama ilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.

Suala hili limejadiliwa bungeni huku kiongozi wa upinzani bungeni Joel Ssenyonyi akitaka kujua kwa nini serikali hailitolei ufafanuzi suala hilo ilhali taarifa zake zimesambaa.

"Vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Serikali vimeripoti wizi katika Benki ya Uganda. Baadhi ya ripoti zimeonyesha Dola za Marekani Milioni 17, hiyo ni takriban Shs62Bn," Ssenyonyi alisema.

"Baadhi ya simulizi zilieleza kwamba kulikuwa na udukuzi uliofanywa na baadhi ya watu huko Asia Kusini na pesa hizo ziliingizwa kwenye akaunti za Asia. Ripoti nyengine zinaonyesha kuwa hii ilikuwa kazi ya ndani ya Benki ya Uganda," aliongezea.

“Serikali yenye dhamana inachofanya ni kutoa tamko la muda, kutuliza umma, kufichua yale ambayo hayataathiri uchunguzi kwa umma, ambao kwa niaba yao, serikali inasema kile inachofikiri sio hatari," alisema Ibrahim Ssemujju mbunge wa Manispaa ya Kira.

Waziri wa Nchi anayeshughulikia Fedha, Henry Musasizi alikubali wakati akijibu hoja iliyotolewa na Joel Ssenyonyi , Kiongozi wa Upinzani ambaye alitaka kujua kwa nini sekta ya Benki ya Uganda imekumbwa na uhalifu huo.

"Nimeona kile kilichoripotiwa na vyombo kadhaa vya habari. Napenda kusema kwamba akaunti zetu zilidukuliwa lakini si kwa kiwango kinachoripotiwa," Waziri Musasizi alisema.

"Hili lilipotokea, tulianzisha ukaguzi na wakati huo huo uchunguzi. Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anafanya ukaguzi na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai wakati huo huo inafanya uchunguzi,” aliongezea Waziri.

Kiongozi wa Upinzani Ssenyonyi alisema kuwa benki nyingine za biashara pia zimeripotiwa kupatwa na matukio kama hayo ya uhalifu katika miezi miwili iliyopita.

Hata hivyo, Waziri wa Fedha wa serikali alikataa kutoa maelezo zaidi ya wizi huo, huku akitoa wito wa uvumilivu na kusubiri matokeo ya mwisho ya ukaguzi na uchunguzi.

"Ili kuepusha upotoshaji wa ukweli, naomba bunge hili kuwa na subira, wakati ukaguzi utakapokamilika. Maafisa wa uchunguzi CID watakapokamilisha uchunguzi, nitakuja bungeni kutoa taarifa," Waziri aliwaambia wabunge.

Hata hivyo, Kiongozi wa Upinzani hakuridhishwa na jibu lililotolewa na Waziri Musasizi, na kumwagiza kufichua kiasi halisi cha pesa zilizoibiwa.

“Hata hivyo, Waziri Musasizi anazungumzia ukaguzi unaoendelea, utaendelea hadi lini? Ni lini tutapata ripoti kama Bunge kuhusu jambo hili? Sababu ya sisi kusisitiza juu ya jambo hili ni kwa sababu, wakati mfumo wa usalama wa mtandao wa Benki Kuu umedukuliwa, ni jambo linalotutia wasiwasi sote," Ssenyonyi alisema.

Waziri wa Fedha alisisitiza kuwa ataleta tena ripoti Bungeni baada ya uchunguzi kukamilika.

TRT Afrika