Serikali Kenya yatahadharisha shule kuhusu ugonjwa wa Mpox

Serikali Kenya yatahadharisha shule kuhusu ugonjwa wa Mpox

Kenya imerekodi jumla ya maambukizi 33 ya Mpox katika sehemu tofauti za nchi.
Moja ya dalili za ugonjwa wa Mpox ni pamoja na kutokwa na vipele mwilini. 

Serikali ya Kenya, inasisitiza jamii kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox hasa katika kipindi hichi ambacho shule zimefunguliwa nchini Kenya.

Hii ni kwa sababu kinga yao bado ni kidogo.

"Wizara ya Afya na ya Elimu zinashirikiana kuongeza elimu ya afya shuleni na kuzipa shule mafunzo mengine muhimu ya kukabiliana na maambukizi ya Mpox," amesema Mary Muthoni, Katibu Mkuu wa wizara ya Afya katika taarifa yake.

Mpaka sasa imerekodi jumla ya maambukizi 33 ya Mpox. Hii ni baada ya kuripotiwa kwa maambukizi manne mapya, huku kaunti ya Nakuru ikiongoza kwa maambukizi 10 na Mombasa ikiwa na maambukizi nane.

Nairobi, Kajiado, Bungoma, Taita Taveta na Kericho zimeripoti kuwa na wagonjwa wawili kwa kila kaunti.

Kaunti za Busia, Makueni, Kilifi, Kiambu, na Uasin Gishu zina mgonjwa mmoja mmoja.

Wizara imetoa maelekezo kwa shule zote kuzingatia usafi huku watoto na walimu wakiombwa kuosha mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji tiririka.

Shule pia zimetakiwa kuanza kufanya utakasaji mara kwa mara ili kuua viini vya maradhi katika madarasa, vyooni na maeneo mengine yanayotumiwa na watoto.

Shule pia zimetakiwa kutoa taarifa ya mtu yeyote atakayeonyesha dalili za joto jingi, vipele, kuvimba sehemu za mwili na kuonyesha uchovu. Serikali imesema kuwa wanafunzi watakaoonyesha dalili hizo wasiruhusiwe kwenda shule mpaka watakapofanyiwa uchunguzi na daktari.

Madarasa yametakiwa kuwa na mazingira mazuri ya kuruhusu hewa.

TRT Afrika