Serikali ya Kenya imesimamisha kibali cha ujenzi wa kituo cha burudani ndani ya msitu wa Karura katika mji mkuu wa Nairobi.
Waziri wa Mazingira Aden Duale amemuamuru Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) Mamo Boru Mamo na Mhifadhi Mkuu wa Misitu Alex Lemarkoko kusitisha leseni iliyotolewa kwa Karura Golf Range Ltd kuiruhusu kuanzisha jengo la burudani ndani ya Msitu wa Ngong Road, Nairobi.
"Nimepata taarifa za kutolewa kwa leseni kwa kampuni ya Karura Golf Range Ltd na Huduma ya Misiti ya Kenya (Kenya Forest Service) tarehe 14 Juni 2023 kwa ajili ya ujenzi wa eneo la mchezo wa gofu na mgahawa katika Hifadhi ya Msitu wa Ngong Road, Kaunti ya Nairobi," Waziri wa Mazingira Aden Duale amesema.
"Pia kuna Leseni ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (IEA) iliyotolewa kwa kampuni iliyotajwa hapo juu na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA) mnamo tarehe 28 Novemba 2024." Waziri ameongezea.
Hatua hiyo imezua utata kwa wananchi na watetezi wa mazingira ambao wamekuwa wakidai kuwa serikali inauza sehemu ya asili.
"Kwa hiyo, nimewaagiza Mhifadhi Mkuu wa Misitu (CCF) na Mkurugenzi Mkuu wa NEMA kusitisha leseni hizo mbili na kuandaa muhtasari wa kina kuhusu suala hilo ndani ya saa 72," Duale amesema.
Msitu wa Karura
Msitu wa Karura uko kaskazini mwa mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Tangu 1932 imetunzwa kama eneo chini ya usalama wa serikali na unasimamiwa kimsingi na Huduma ya Misitu ya Kenya.
Kimsingi ni hifadhi ya msitu wa mjini na nafasi ya kijani ndani ya jiji.
Msitu wa karura upo katika eneo la takriban hekta 1,041.
Waziri wa Mazingira ameagiza Huduma ya Misitu ya Kenya kutotoa leseni zozote maalum za ziada na Ukaguzi wa leseni zote zilizotolewa hapo awali utafanywa kwa wakati ufaao ili kuhakikisha uwazi na uwajibikaji.
"Bodi ya KFS ilikuwa imeidhinisha kutolewa kwa Leseni ya Matumizi Maalum mnamo 2022, kwa ajili ya kuendeleza uwanja wa gofu na mkahawa katika mtaa wa Miotoni, Msitu wa Ngong Road, ndani ya njia ya bomba la mafuta," Huduma ya Misitu ya Kenya imejitetea katika mtandao wa X.
"Kampuni ya mafuta ya Kenya yaani Kenya Pipeline haikuonyesha pingamizi lolote kwa safu ya gofu iliyopendekezwa, na NEMA ikatoa cheti cha kufuatia mchakato ambao pia ulijumuisha ushiriki wa umma. Hakuna miti ambayo ingeathiriwa na leseni hii wakati wa utekelezaji wa masharti ya leseni," imeongezea.
Uvamizi huu wa hivi punde katika Msitu wa Ngong unajiri siku chache baada ya kilio cha umma kuzuka kuhusu Huduma ya Misitu ya Kenya kuidhinisha ruhusa ya ekari 51.64 katika Msitu wa Karura, iliyopewa Mamlaka ya Kitaifa ya Barabara Kuu (KeNHA) kwa ajili ya upanuzi wa Barabara ya Kiambu.