Seneta wa Kenya amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi na matumizi mabaya ya ofisi zinazohusisha pesa zilizokusudiwa kuwafadhili wanafunzi wa Kenya kuendelea na masomo nchini Finland na Canada.
Seneta Jackson Mandago pamoja na washukiwa wengine wawili waliachiliwa Alhamisi kwa dhamana ya pesa taslimu na mahakama katika mji wa kati wa Nakuru wakisubiri kesi yao kusikilizwa.
Wanashutumiwa kwa kuhusika na mpango wa kuwahaidi watu ufadhili wa masomo ambao inadaiwa hawakupata. Takriban dola $7.6 zililipwa na wazazi waliotaka watoto wao kwenda kusoma ulaya.
Makumi ya wanafunzi wanadaiwa kusalia nchini Kenya licha ya pesa kulipwa kwa mpango wa elimu, vyombo vya habari vya ndani vinaripoti.
Wazazi wengine wamesimulia vile walilazimika kuuza mali yao kama mifugo na shamba ili kupata fedha kwa ajili ya mpango huo.
Malipo hayo yalifanywa kipindi ambapo Mandago alikuwa gavana wa kaunti ya Uasin Gishu.
Hapo awali alikanusha makosa yoyote na Jumatano alisema kuwa alikutana na "uongozi wa wazazi wanaodai kurejeshewa pesa na walikubaliana mfumo wa malipo". Mandago alisema katika akaunti yake ya X ( Twitter)
Mzozo huo ulishuhudia Rais William Ruto Jumatano akitoa wito kwa wahusika kuwajibika.