Na
Brian Okoth
Senegal imetoa makataa kwa mwanamuziki Akon kuanza kujenga kwenye eneo la ekari 136 alilopewa mwaka wa 2020, au asilimia 90 ya ardhi itarejeshwa kwa serikali.
Miaka minne iliyopita, Senegal ilitoa ardhi kwa Akon kuendeleza jiji lenye huduma zikiwemo hospitali, mapumziko, chuo kikuu, bustani ya burudani, maduka makubwa, kituo cha polisi, mtambo wa nishati ya jua na vyumba.
Ardhi hiyo iko katika eneo la pwani la Mbodiene, kilomita 120 kusini-mashariki mwa mji mkuu wa Senegal, Dakar.
Akon aliahidi kuanza ujenzi wa ardhi hiyo haraka iwezekanavyo, akiwa na uundaji wa nafasi za kazi na kukuza uchumi wa Senegal kichwani mwake.
Mradi wa mabilioni ya dola
Mwanamuziki huyo mwenye asili ya Senegali na Marekani alisema awamu ya kwanza ya mradi huo, unaogharimu dola za kimarekani bilioni 6, ingekamilika mwaka wa 2023.
Tarehe ya kukamilika, hata hivyo, iliahirishwa hadi 2025, huku Akon akitaja janga la COVID-19 kama sababu ya kuchelewesha ujenzi.
Sehemu iliyosalia ya jiji ilipaswa kujengwa hatua kwa hatua, na tarehe ya kukamilika kwa mradi wote iliwekwa kuwa 2030.
Akon alisema kuwa baada ya kukamilika, jiji hilo litakuwa "sehemu salama kwa Waamerika wenye asili ya Afrika wanaotaka kuunganishwa na asili yao ya Kiafrika."
Mipango iliyokwama
Hata hivyo, eneo hilo bado halijaendelezwa, huku mifugo mara nyingi ikionekan kual nyasi.
Kizuizi kimoja tu cha zege kinachoashiria msingi wa mradi kinaweza kuonekana mahali hapo.
Hatua hiyo imezua hisia kali mtandaoni, kuanzia wale wanaounga mkono jitihada ya serikali ya kutwaa tena milki yake hadi na wale wanaoipinga.
"Akon hana kiasi hicho cha pesa kufadhili mradi mkubwa kama huo. Usiruhusu mtu yeyote akudanganye. Serikali inafaa kutwaa ardhi hiyo na kuiendeleza," mwanablogu wa mitandao ya kijamii Ynsson alisema kwenye TikTok.
Mwingine, Nelly Viano, hata hivyo, alipendekeza mradi huo usiharakishwe. "Mpeni mtu muda. Afrika ina umri gani tena ambao nyote mnatarajia mtu mmoja kufanya miujiza.? Inachukua muda kufikia mambo haya."
Victor_official anakubali, akisema Akon anahitaji kuungwa mkono na sio kukosolewa.
"Hizi ni baadhi ya sababu kwa nini Afrika bado iko nyuma; hatujiamini na hatujisaidii. Hata Burj Khalifa inajengwa na serikali ya Dubai na wawekezaji wa kimataifa. Mpe Akon nafasi."
Tuma malipo
Senegal, kupitia kampuni ya maendeleo ya maeneo ya pwani ya kitalii ya SAPCO, imetishia kutwaa ardhi hiyo, ikisema Akon ameshindwa kutuma malipo ya kumiliki ardhi hiyo.
Mwimbaji, hata hivyo, hana hati miliki ya ardhi. Timu ya Akon inadai juhudi zinaendelea za kusafisha na kuchora ramani ya ardhi kwa ajili ya ujenzi uliopangwa.
Mwishoni mwa 2023, Akon alisema katika mahojiano na BBC kwamba mradi wake nchini Senegal "unasonga asilimia100,000" na kwamba wakosoaji wake wataaibika.
Hata hivyo, watu kadhaa katika kijiji cha Mbodiene wamepoteza matumaini katika mradi huo.
Akon mwenye umri wa miaka 51 alikuwa anategemea wawekezaji ili kukusanya rasilimali kwa ajili ya ujenzi wa jiji hilo, lakini kulingana na timu ya Akon, "ahadi za uwekezaji" hazikutekelezwa.
Julius Mwale wa Kenya alikuwa ametajwa kuwa mwekezaji mkuu wa mradi huo.
Thamani ya Akon haijulikani, lakini ripoti kadhaa zinaonyesha kuwa inaweza kuwa kati ya dola milioni 40 hadi 80 za Kimarekani.
Akon City ya Uganda
Huku hatima ya Akon City nchini Senegal ikining’inia, hali ya sintofahamu imetanda pia nchini Uganda, ambapo serikali ilimpa Akon ardhi ya ekari 640 kujenga jiji lenye thamani ya dola bilioni 6 za Marekani.
Ardhi hiyo ilipendekezwa kwa Akon baada ya kukutana na Rais Yoweri Museveni nchini Uganda mnamo Aprili 2021.
Wakaazi wa mji wa Mukono katikati mwa Uganda, ambako mradi huo umepangwa, hata hivyo, wamekataa hatua ya serikali ya kumpa ardhi Akon, wakisema ni milki ya mababu zao.
Kama ilivyo nchini Senegal, ujenzi wa Akon City nchini Uganda bado haujaanza.
Wazazi wa Akon ni wa kutoka Senegal, ambao baadaye walihamia New Jersey nchini Marekani.