Ramadhan Kibuga
TRT Afrika, Bujumbura, Burundi
Marais wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, wamekutana Jumanne usiku kwa njia ya mtandao kuzungumzia hali ya usalama Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Marais hao watakutana tena baadaye siku ya Jumamosi tarehe 4 Novemba 2023 katika kikao chengine mjini Luanda nchini Angola.
Lengo la mkutano huo ilikuwa ni kukamilisha mpango wa kupeleka vikosi vya kijeshi hivi karibuni nchini DRC (SAMIDRC).
Mpango huo umekuwa kwenye meza ya majadiliano kuanzia mwezi Mei mwaka huu.
Viongozi wa DRC wanaamini kwamba kupeleka vikosi vya SADC nchini humo imekuwa ni suala la muda tu.
Na inaelezwa tayari kuwa ya baadhi nchi zilishatangaza nia ya kutuma vikosi vyake nchini Congo.
Afrika Kusini, Malawi, Tanzania na Angola kwa upande wake, wamesalia na msimamo wa awali: kupeleka majeshi Mashariki mwa DRC, lakini kwanza kuhakikisha umemalizika mpango wa kuwakusanya waasi wa M23.
Mkutano wa Marais wa baadaye Jumamosi hii utakuwa ni fursa ya kuweka mikakati ya mwisho baada ya vikao vingi kwenye ngazi ya wakuu wa majeshi pamoja na mawaziri.
Ratiba inapangwa
Ratiba ya kupeleka vikosi vya SADC bado haijapangwa.
Lakini viongozi wa DRC wanasema wangependa kuona mpango huo unafanyika kwa haraka kwa sababu muda wa vikosi vya Afrika ya Mashariki umefikia kikomo chake baadae mwishoni mwa mwezi Disemba.
Hata hivyo mpango huo wa kuyapeleka majeshi ya SADC unaibua maswali mingi kwa wadadisi wa mambo ya siasa za Congo.
''Itakuwa vigumu kuona jinsi mpango huo utavyotekelezwa maana sehemu kubwa ya nchi hizi za ukanda zimekuwa na maslahi ambayo yanakinzana kuhusu Mashariki mwa DRC, '' amesema Dk Abdoul Djumaine, mchambuzi wa siasa za Maziwa Makuu.
Vikosi vya EAC kuondoka
Jeshi la Kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) ni kikosi cha kimataifa kilichotumwa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mnamo Novemba 2022 kusaidia amani kurejea katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
EACRF ilitumwa katika maeneo ya Masisi, Nyiragongo na Rutshuru huko Kivu Kaskazini, ambako imekuwa ikifanya kazi kwa ushirikiano na Jeshi la DRC (FARDC) kusaidia mchakato wa kisiasa, ulinzi wa raia na kutekeleza makubaliano ya amani.
Changamoto kubwa katika eneo hilo ni kikundi cha M23, kikundi chenye silaha ambacho kiliundwa takribani miaka 10 iliyopita.
Kikundi cha M23 kimechukua maeneo makubwa ya eneo la mashariki, kikidai kutetea maslahi ya kabila la Watutsi dhidi ya wanamgambo wa Kihutu ambao linasema wanaungwa mkono na serikali.
Mwezi Septemba marais wa Afrika Mashariki waliamua kuongeza awamu ya kikosi hicho nchini DRC hadi Disemba tarehe 8 .
Lakini serikali ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilitangaza kwamba haina imani tena na vikosi hivyo vya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki .
Imesema mara nyingi kwamba vikosi hivyo vimeshindwa kutekeleza majukumu yake katika eneo la Mashariki mwa Congo hasa kwa kushindwa kulidhibiti kundi la waasi wa M23.
Rais wa DRC Felix Tshisekedi amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa kikosi hicho. akidai wana "ukosefu wa ufanisi" na waambia wachukua hatua kali zaidi dhidi ya M23 au kuondoka nchini.
Hayo yanaarifiwa wakati DRC inajiandaa kwa uchaguzi mkuu baadaye mwezi wa Disemba mwaka huu.