Rwanda imesema bado inadumisha hatua za kujihami zilizowekwa kukabiliana na tishio la usalama kutoka nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, DRC.
Olivier Nduhungirehe Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. amesema itaendelea kufanya hivyo hadi pale makubaliano ya kuwaangamiza wanamgambo wa FDLR yatakapotimia.
FDLR ni mojawapo ya makundi makubwa ya kigeni yenye silaha katika eneo la DRC. Kundi hilo liliundwa mwaka wa 2000, na limehusishwa na baadhi ya watu waliofanya mauaji ya kimbari nchini Rwanda 1994, na wakakimbilia nchi jirani ya DRC.
Waziri alisema Rwanda inaendelea kukabiliwa na vitisho na matamshi ya chuki kutoka kwa maafisa wa DRC, licha ya makubaliano yaliyotiwa saini 25 Novemba 2024 nchini Angola kuhusu dhana ya operesheni (CONOPS), ambayo ingeongoza kusambaratishwa kwa FDLR na Rwanda kuondoa hatua za kujihami kwenye mpaka wake na DRC.
Mawaziri wa mambo ya nje wa Rwanda na DRC wakiwa na upatanishi wa Angola, 25 Novemba 2024, walijadili rasimu ya makubaliano kuhusu hali ya amani na usalama mashariki mwa DRC iliyotiwa saini katika mji mkuu wa Angola Luanda.
Mkutano huo ulikuwa na nia ya kuanza tena mjadala kuhusu rasimu ya makubaliano kati ya Rwanda na DRC kuhusu kurejesha amani na utulivu mashariki mwa DRC na kukuza uhusiano wa kindugu kati ya nchi mbili hizo.
"Kwa vyovyote vile, ili kutekeleza makubaliano haya ya amani makubaliano tuliyotia saini, tunahitaji nia njema," Nduhungirehe alisema katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la taifa la Rwanda RBA.
"Tumesema kwa nyakati tofauti kwamba tuna hatua za kujihami katika mpaka na DRC kukabiliana na tishio hilo la usalama. Na hatua hizo ni za nguvu na zinalingana na tishio ambalo tunakabiliana nalo," alisema.
Waziri huyo alisema matamshi ya "kashfa" ya maafisa wa serikali ya DRC yanaendelea kudhoofisha juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, ambao ulichafuliwa na shutuma kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 katika jimbo la Kivu Kaskazini. Rwanda siku zote imekuwa ikipinga tuhuma hizo.
Nduhungirehe alisema matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Sheria wa DRC Constant Mutamba mnamo 24 Novemba 2024, kutishia "kuwaua Banyarwanda" na viongozi wa Rwanda hayakusaidia juhudi za kurejesha uhusiano wa kawaida au kumaliza mateso kwa jamii ya Watutsi walio DRC.
Mutamba, ambaye alikuwa akizungumza na wafungwa katika gereza la Munzenze huko Goma, jiji lililo mpakani na Rwanda, aliwataka wafungwa kutoa taarifa za mtu yeyote mwenye uhusiano na "wasaliti."
"Yeyote anayewasiliana na Banyarwanda atakamatwa na kuuawa," Mutamba alisema, akiahidi kuwaachilia wafungwa ambao wangetoa taarifa za wale waliotambuliwa kama wasaliti.
Makubaliano ya Luanda
Waziri wa Rwanda amesema nchi hizo mbili zina changamoto tatu za kiusalama: kikundi cha FDLR, hatua za ulinzi na waasi wa M23. Amesema masuala mawili ya kwanza yalishughulikiwa kwa njia fulani katika mkutano wa mwezi uliopita huko Luanda.
"Lakini kuna suala lililosalia la waasi wa M23 ambalo linapaswa kushughulikiwa pia. Tumetoa pendekezo na tunaamini kwamba kabla ya kutia saini makubaliano yoyote na DRC suala hili linahitaji kushughulikiwa," Nduhungirehe ameongezea.
"Kwa Rwanda, tumekuwa wazi kwamba kuna haja ya kujitolea kwa DRC kushiriki katika mazungumzo ya moja kwa moja na M23, kwa nia ya kutafuta suluhu la kudumu ya mgogoro huu."
"