Ikiwa Marburg haina chanjo ya moja kwa moja dhidi yake au matibabu, dozi za chanjo ambayo Rwanda inapokea ni za uchunguzi / Picha: Wizara ya afya Rwanda

Rwanda imepokea chanjo 1000 zaidi kutoka kwa Kampuni ya Sabin Vaccine ili kupambana na maambukizi ya Marburg.

Ikiwa Marburg haina chanjo ya moja kwa moja dhidi yake au matibabu, dozi za chanjo ambayo Rwanda inapokea ni za uchunguzi.

"Tumetoa chanjo kwa zaidi ya watu 600 kati ya 700 tuliopokea, na jana tu, tulipokea dozi 1,000 za ziada," Waziri wa Afya Dkt. Sabin Nsanzimana alisema.

Chanjo zinalenga wafanyakazi wa afya na wale walio katika mazingira hatarishi, hasa wale wanaofanya kazi katika vitengo vya wagonjwa mahututi (ICUs) ambao wanakabiliwa zaidi na hatari ya maambukizi.

"Tukiwapa chanjo mapema ndivyo bora kwa afya zao na usalama wa umma," Waziri alisema.

Dozi hizi zinaongezea na nyengine 700 ambazo nchi hiyo ilipokea Oktoba 5, siku tisa baada ya mlipuko wa Marburg kuripotiwa nchini humo Septemba 27, 2024.

Waziri alisema kuwa mpango wa sasa wa chanjo upo katika awamu ya pili, ukilenga ufanisi tofauti na awamu ya kwanza wa chanjo iliyolenga usalama.

Rwanda ilianza kutoa chanjo kwa wafanyakazi wa afya walio mstari wa mbele Oktoba 6 kama sehemu ya majibu yake ya haraka.

Kufikia Jumamosi, dozi 620 kutoka usambazaji wa awali zilikuwa tayari zimetolewa.

Chanjo ya dozi moja ya kampuni ya Sabin inasambazwa kwa mujibu wa itifaki ya kimatibabu iliyoidhinishwa na Mamlaka ya Maadili na Udhibiti ya Rwanda.

Tangu Septemba 27, maambukizi 61 ya virusi vya Marburg yamethibitishwa, watu 14 wamekufa na watu 29 wanaendelea na matibabu.

TRT Afrika