Rwanda imelishutumu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kwa kuwasilisha madai ya uwongo kwa mahakama za Uingereza kuhusu namna nchi hiyo inavyowatendea wanaotafuta hifadhi huku kukiwa na wasiwasi kuhusu mkataba wa uhamiaji ambao Uingereza ilitia saini na Kigali.
Shutuma hizo zilikuja Jumanne, siku moja baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kuwaonya majaji wa Uingereza kwamba linaweza kuwa na ushahidi mpya kuanzia 2024 kwamba Rwanda imehatarisha maisha ya wanaoomba hifadhi.
UNHCR iliiambia Mahakama Kuu Jumatatu kwamba inachunguza madai mapya ya unyanyasaji na watu ambao wanaweza kupelekwa katika nchi ambayo wanaweza kuteswa.
Jaji ametoa ruhusa kwa UNHCR kuandaa ripoti kabla ya ndege ya wanaotafuta hifadhi kuondoka Uingereza.
Rwanda yasema UNHCR haisemi ukweli
Taarifa ya ofisi ya msemaji wa serikali ya Rwanda ilisema "UNHCR inadanganya."
Ilisema moja ya kesi ambazo UNHCR imerejelea inahusiana na ya mtu ambaye alinyimwa hifadhi huko Ushelisheli, na shirika hilo liliamua kwa upande mmoja apewe hifadhi Kigali bila kushauriana na mamlaka.
"Shirika linaonekana kudhamiria kuwasilisha madai ya uwongo kwa mahakama za Uingereza kuhusu nchi hiyo kwa wanaotafuta hifadhi, huku likiendelea kushirikiana nasi kuwaleta wahamiaji wa Kiafrika kutoka Libya hadi salama nchini Rwanda kupitia njia ya dharura," ilisema taarifa hiyo.
"Kama tulivyosema mara kwa mara, Rwanda haiwapingi watu wanaotafuta hifadhi. UNHCR inaonekana kuwa na nia ya kudhoofisha usalama wa Rwanda ndani ya mahakama za Uingereza."
Uingereza ilifikia makubaliano yanayodaiwa kuwa na utata ya uhamiaji na Rwanda mnamo Aprili 2022. Makubaliano hayo yangerahisisha kutuma baadhi ya wahamiaji wanaofika Uingereza hadi nchi hiyo ya Afrika Mashariki, ambapo madai yao ya hifadhi yangeshughulikiwa.
Mwezi Aprili, wabunge wa Uingereza walipitisha Mswada wa Usalama wa Rwanda huku kukiwa na ukosoaji wa vyama vya upinzani na mashirika ya misaada yanayowakilisha waomba hifadhi.
Sheria hiyo ilianzishwa ili kuzuia uamuzi wa Mahakama ya Juu ambao ulisema mpango huo ulikuwa kinyume cha sheria.
Vyombo vya habari vya Uingereza vinaonyesha kuwa hakutakuwa na safari za ndege kabla ya angalau Julai 24 na Waziri Mkuu Rishi Sunak amesema safari za ndege zitaendelea mara tu atakapochaguliwa tena.