Uingereza inaishtumu serikali ya Rais Paul Kagame kwa kuunga mkono kikundi chenye silaha cha M23 / Picha:  AFP

Rwanda imelalamika vikali kuhusu vikwazo vilivyotangazwa na Serikali ya Uingereza katika kukabiliana na mzozo wa mashariki mwa DRC.

" Vikwazo vilivyotangazwa leo na serikali ya Uingereza katika kukabiliana na mzozo wa mashariki mwa DRC - ambapo sasa Uingereza inaegemea upande mmoja - havifai," Wizara ya Mambo ya Nje ya Rwanda ilisema katika taarifa.

Uingereza inaishtumu Rwanda kuunga mkono kikundi chenye silaha cha M23, ambacho tangu Januari kimefanya mashambulizi mengine mashariki mwa DRC na kinaripotiwa kuendelea kudhibiti miji Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Lakini Rwanda inaendelea kukanusha madai haya.

" Serikali ya DRC inatakiwa iijibu maswali mengi kuliko kundi lingine lolote ndani ya DRC yenyewe na kanda nzima, lakini haiwajibishwi kwa kukiuka haki za msingi za watu wake kwa sababu ambazo zinafahamika wazi," Rwanda imeongeza.

Vikwazo kutoka Uingereza ni pamoja na Maafisa wa ngazi za juu wa nchi hiyo kutohudhuria mikutano yoyote ambapo Rwanda ni mwenyeji, kupunguza shughuli za biashara na Rwanda, kusitisha usaidizi wa kifedha kwa Rwanda, pamoja na kusimamisha mipango yoyote ya kusaidia taifa hilo katika mafunzo ya kijeshi. Uingereza pia imesema itaangalia upya tena leseni ya mauzo ya nje ya jeshi la Rwanda.

" Kutokuwajibisha Serikali ya DRC kwa mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia wake, ikiwa ni pamoja na kuwashambulia kwa mabomu watu katika vijiji vya Banyamulenge huko Kivu Kusini, kunawapa nguvu DRC kuendelea na mapigano ya kijeshi, kuendeleza migogoro na mateso kwa raia," imeongeza.

Rwanda inasema haitokubali kuhatarisha usalama wake pamoja na raia wa nchi hiyo. Mbali na Uingereza, Februari 24, bunge la mataifa ya Ulaya lilijadili uwezekano wa kuiwekea Rwanda vikwazo.

Wabunge walifikia makubaliano ya awali tu wakisema maamuzi yanatakiwa kuchukuliwa kulingana na kutathmini hali inavyoendelea nchini DRC. Bunge hilo lilipinga vikwazo kwa Rwanda likidai ni vyema kusubiri kufahamu matokeo ya mchakato wa amani unaoongozwa na Umoja wa Afrika.

Iwapo kutakuwa na vikwazo kutoka Umoja wa Ulaya basi itamaanisha kusitishwa kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Rwanda na EU. Umoja huo wa Ulaya ulitoa Euro milioni 20 kufadhili kikosi cha Rwanda cha kulinda amani huko Cabo Delgado, nchini Msumbiji.

Pia itaamanisha msaada wa maendeleo na makubaliano katika sekta ya madini utasitishwa wakati huo huo, Marekani imemuwekea vikwazo James Kabarebe, mshauri mkuu wa masuala ya kijeshi wa rais wa Rwanda Paul Kagame, ikimhusisha na waasi wa M23.

Rwanda inasisitiza kuwa hatua hizo za vikwazo hazisaidii chochote katika kupata suluhu ya mzozo wa Mashariki mwa DRC.

Serikali ya Rais Paul Kagame inasema imejitolea kikamilifu kufanya kazi na washirika katika mchakato unaoendelea wa upatanishi unaoongozwa na Umoja wa Afrika. Pia inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi hizi.Rwanda inaamini hii ndiyo njia pekee itakayomaliza matatizo ya DRC.

TRT Afrika