Rwanda imeanza safari ya kuondoa katika matumizi pikipiki zinazotumia mafuta kwa nia ya kusafisha mazingira na hewa yake.
“Hatutasajili pikipiki za petroli kwa usafiri wa umma mjini Kigali. Ni zile za umeme pekee ndizo zitakazozingatiwa kwa usafiri wa umma wa kibiashara,” Jimmy Gasore, Waziri wa Miundombinu aliwaambia waandishi wa habari wa nchi hiyo.
Kuanzia mwaka 2025, Serikali imesema pikipiki ambazo hazitumii nishati ya umeme hazitasajiliwa.
Waziri alifafanua kuwa sera hiyo haitaathiri pikipiki zilizopo zinazotumia mafuta ya petroli, ambazo zitaendelea kufanya kazi bila usumbufu.
"Hii ndiyo sababu hatutarajii athari mbaya za kiuchumi," aliongeza.
Hatua hii pia inakatisha tamaa uagizaji wa pikipiki zisizo za umeme kwa usafiri wa umma, kulingana na mkakati mpana wa Rwanda wa uhamaji wa kielektroniki.
Juliet Kabera, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira ya Rwanda (REMA), alisisitiza faida za kimazingira, akibainisha kuwa pikipiki za umeme zinachangia kutotoa hewa chafu.
"Tayari kuna wachezaji wengi katika mfumo wa ikolojia wa pikipiki za umeme. Baiskeli za umeme ni rafiki kwa mazingira na bei nafuu,” Kabera alisema, akirejelea mradi wa majaribio ambapo pikipiki za petroli ziliwekwa upya na vipengele vya umeme, kubadilisha injini, moshi, na cheni za umeme.
Mnamo Juni 2021, Rwanda, kwa ushirikiano na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP), ilianza hatua kwa hatua ya kuondoa pikipiki zinazotumia petroli kwa kuhimiza ubadilishaji mbadala wa umeme, ikilenga kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi na uchafuzi wa hewa.
Wakati huo, zaidi ya pikipiki 100,000 zilisajiliwa nchini kote, na 46,000 zikitumika kama boda boda zikiwemo 26,000 jijini Kigali pekee.
Serikali inasema pikipiki hizi huchangia kwa kiasi kikubwa katika ubora duni wa hewa na uharibifu wa mazingira.
Nchi nyengine pia zimeonyesha nia kama ya Rwanda. Kwa mfano, mwaka 2023 Rais wa Kenya William Ruto alivumbua kiwanda ambacho kinatengeza pikipiki za umeme akisema kuwa matumizi ya pikipiki hizo yatahimizwa kwa ajili ya kuchangia hewa safi nchini.