Rwanda inalenga kuongeza uzalishaji wa nyama kutoka tani 207,097 kwa mwaka 2023/24 hadi tani 247,223 kufikia mwaka wa fedha 2028/29.
Mpango huo, ni sehemu ya mkakati wa mageuzi katika sekta ya kilimo (PSTA5), kulingana na takwimu iliyotolewa na Bodi ya Maendeleo ya Kilimo na Rasilimali za Wanyama (RAB).
Takwimu hiyo pia inaonesha ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hiyo kwa asilimia 20 ndani ya miaka mitano.
Kwa mujibu wa Solange Uwituze, ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa rasilimali za wanyama katika bodi ya RAB, Rwanda ilifanikiwa kufikia uzalishaji wa nyama wa tani 207, 097 kwa mwaka wa fedha 2023/24, ambayo ni sawa na asilimia 96.3 ya lengo la tani 215,058 lililowekwa na PSTA.
Hata hivyo, Uwituze alisema kuwa kipindi kirefu cha ukame kilichoshuhudiwa mwaka wa fedha 2023/24 kiliathiri upatikanaji wa wa ng’ombe.
“Ng’ombe walikuwa adimu kutokana na hali mbaya ya hewa na hivyo kusabisha uzalishaji mdogo wa nyama,” alisema.
Kulingana na Uwituze, gharama kubwa za chakula cha mifugo, pia kilichangia kushuka kwa uzalishaji wa nyama ya ng’ombe.