Peter Mutharika mwenye umri ya miaka 84 alikuwa rais wa Malawi kuanzia 2014 hadi 2020 / Picha: AFP

Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi, Democratic Progress Party kilitanaza siku ya Jumapili ya kuwa Rais wa zamani Peter Mutharika ndiye mgombea wake katika uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Mutharika, 84, ambaye alikuwa rais kuanzia 2014 hadi 2020, alisema katika hotuba yake ya kukubali chaguo la chama chake, kuwa watarekebisha uchumi ambao amesema umekuwa wa upungufu wa fedha na kukabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni uliosababisha ukosefu wa mafuta na dawa.

Atakabiliana na Rais Lazarus Chakwera wa Chama cha Malawi Congress, ambaye atawania muhula wa pili katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Septemba 16, 2025.

"Tuna uzoefu wa kushinda kutoka kwa upinzani. Tutafanya vivyo hivyo mwaka ujao. Tunakuja kurekebisha uchumi," Mutharika aliuambia mkutano mkuu wa chama chake katika mji mkuu wa kibiashara wa Blantyre.

Mutharika, profesa wa zamani wa sheria, alisimamia uboreshaji wa miundombinu na kupungua kwa mfumuko wa bei wakati wa uongozi wake, lakini wakosoaji walimtuhumu kwa ufisadi, jambo ambalo anakanusha.

Chakwera, 69, aliingia madarakani akiahidi kukabiliana na ufisadi na kuharakisha ukuaji wa uchumi, lakini wapinzani wake wanasema hajafanikiwa kwani uchumi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika bado ni tete.

Mutharika alisema ataunda muungano wa upinzani kikiwemo cha United Transformation Movement, chama kilichoasisiwa na hayati Makamu wa Rais Saulos Chilima aliyefariki katika ajali ya ndege mwezi Juni.

Chama cha UTM kilimsaidia Chakwera kumshinda Mutharika mnamo 2020, lakini baada ya kifo cha makamu wa rais kilitangaza nia yake ya kujiondoa kwenye muungano unaotawala.

UTM bado haijathibitisha muungano na chama cha Mutharika, ambacho kingebadilisha sana kinyang'anyiro hicho. Msemaji wa UTM hakujibu ombi la maoni.

TRT Afrika