Rais wa Sudan Kusini asema nchi yake haitarudi katika vita

Rais wa Sudan Kusini asema nchi yake haitarudi katika vita

Matamshji ya Rais Salva Kiir yanafuatia uvumi wa kuwepo mzozano kati ya wanajeshi.
Rais Salva Kiir amewahakikishia raia wake utulivu nchini humo licha ya kuwepo kwa uvumi wa jeshi kuzozana. 

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amelihakikishia taifa lake kuwa halitarudi katika vita tena. Taarifa yake inafuatia kuwepo kwa taarifa za uvumi za jeshi la nchi hiyo kuzozana.

"Nikiwa Rais wenu, niko hapa kuwahakikishia kuwa nchi yetu iko salama. Narudia tena kusema kuwa nchi yetu haitarudi vitani. Tutakumbatia mazungumzo ili kutatua tofauti zetu," Rais Kiir aliwaambia wananchi wake.

"Niko hapa kuzungumzia hofu na mvutano uliotokea 26 Novemba 2024, taarifa potofu zinazosambazwa kuhusu mgogoro katika makao makuu ya jeshi ni za uongo," Rais Kiir alisema.

Sudan Kusini kwa sasa inaongozwa na serikali ya mpito huku Rais Salva Kiir akiongoza na makamu wake ni Riek Machar/  Picha: AFP

Ameliambia taifa lake kuwa jeshi la nchi lipo sawa na pamoja na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama vinatekeleza majukumu yao ya kizalendo ipasavyo.

Sudan Kusini inaendelea kujikwamua kutokana na athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza Disemba 2013.

Wakati huo wanajeshi waligawanyika huku wanaomuunga mkono Rais Salva Kiir wakipigana na wale waliokuwa wanamuunga mkono aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo Riek Machar.

Hii ilizua vita vya kikabila kati ya kabila la Dinka ambalo ni asili ya Rais Salva Kiir na Nuer ambalo ni asili ya Machar.

Zaidi ya watu milioni 2.3 walikimbilia nchi jirani za Ethiopia, Sudan na Uganda.

Pande zinazozozana zilifanya makubaliano ya amani yaliyosaidia kuundwa kwa seriklai ya mpito iliyoanza kazi Februari 22, 2020 ikiwa uongozi umegawanywa kati ya Rais Salva Kiir, na aliyekuwa mpinzani wake Riek Machar na vikundi vyengine.

Kati ya masharti ya makubaliano haya ni kuwepo kwa mikakati ya umoja wa majeshi, huku vikundi vilivyokuwa vinapinga serikali vikitakiwa kuleta majeshi yao yawe chini ya jeshi la taifa.

TRT Afrika