Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa Leseni za Udereva utakaoweza kuwapunguzia alama (points) madereva wanaofanya makosa kwa uzembe/ Picha: Wengine.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameliagiza Jeshi la Polisi nchini humo kuwa na mfumo wa kuwaadhibu madereva wanaofanya uzembe barabarani.

"Nimeliagiza Jeshi la Polisi kuwa na mfumo wa Leseni za Udereva utakaoweza kuwapunguzia alama (points) madereva wanaofanya makosa yenye kuhatarisha usalama na uhai barabarani," Rais Suluhu alisema katika salamu zake za rambi rambi baada ya ajali ya barabarani katika eneo la Mikese, Barabara Kuu ya Morogoro - Dar es Salaam.

Usiku wa kuamkia Disemba 18, 2024 watu 15 walifariki katika ajali ya barabarani, iliyohusisha gari ya mizigo na gari la abiria aina Coaster.

Idadi ilifika 15 baada ya mtoto wa miaka nane kupoteza maisha wakati akifanyiwa upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya Morogoro.

Maagizo mapya ya Rais yanafuatia wito wa Rais Suluhu kwa umma na maelekezo aliyoipa Jeshi la Polisi na vyombo vya usalama Disemba 4 mwaka huu kuhusu kuongeza umakini na usimamizi katika Sheria za Usalama Barabarani.

"Mfumo huu uweke taarifa (records) kielektroniki za mwenendo wa makosa ya madereva barabarani kitakwimu, na kisha utumike kuamua kama wanastahili kuendelea kuwa na leseni za udereva au la. Hii ni katika kuboresha mfumo wa sasa ambao mara nyingi dereva hulipa faini pekee na kuachwa kuendelea kuwepo barabarani," Rais ameongezea katika ujumbe wake kupitia X.

Rais Samia amesema ni lazima kuendelea kuchukua hatua za pamoja na madhubuti kuhakikisha uhai wa wananchi unalindwa kwa njia zote.

"Hatua hizi ni pamoja na kuhakikisha vyombo vya moto vinavyoingia barabarani vina sifa na vigezo vya kutumia barabara, na wale wanaoviendesha wana sifa, vigezo na rekodi za kustahili kuendelea kufanya hivyo," Rais Suluhu amesema.

Dkt. Daniel Nkungu Afisa Mkuu wa Afya wa hospitali ya rufaa ya Morogoro alisema Jumatano kwamba tayari watu watano kati ya 15 waliofariki walikuwa tayari wametambuliwa na familia zao. Amesema wengine saba waliojeruhiwa bado wanapata matibabu katika hospitali.

TRT Afrika