Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake inapanga mkakati wa kuifanyia kazi changamoto ya ndovu wanaoharibu na kujeruhi wananchi hasa katika mkoa wa Lindi, kusini mwa Tanzania.
Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara punde tu baada ya kuweka Jiwe la Msingi kwenye ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Lindi iliyopo katika kijiji cha Mitwero.
Mbali na maeneo ya kusini mwa Tanzania kuwa na changamoto ya ndovu wanaovamia makazi na kuhatarisha usalama wa watu pamoja na kuharibu mali ikiwemo mazao, mikoa kama Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Arusha kwa kanda ya kaskazini, na mkoa wa Morogoro nayo pia inakabiliwa na tatizo hilo.
Ongezeko la shughuli za binadamu hasa katika maeneo ambayo ni mapitio ya wanyama hao, imeelezwa kuwa moja wapo ya sababu za uvamizi huo.
Idara ya wanyama pori nchini Tanzania inasema ongezeko la idadi ya ndovu pia inachangia kuwepo kwa tatizo hilo.
Tanzania inakisiwa kuwa na idadi ya ndovu elfu 60 tofauti na miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, wananchi mara kadhaa wamekuwa wakiilalamikia serikali kutochukua hatua madhubuti kutokana na malalamiko yao.