Rais William Ruto amesema kuwa serikali haitakubali mambo ya vurugu kutoka kwa maandamano.
Kinara wa upinzani Raila Odinga alitangaza maandamano ya siku tatu kutoka Jumatano, dhidi ya sera za rais Ruto ambazo zinanuia kuongeza ushuru.
"Tumemkalia ngumu jana, leo na kesho." Rais Ruto alisema akiwahutubia wananchi katika ziara yake katika eneo la Meru nchini Kenya.
Serikali ilitangaza kuwa maandamano hayo ya siku tatu si halali. Lakini kuna wale ambao walijitokeza katika sehemu tofauti ya nchi.
"Hatuna Kenya ingine, Kenya ni hii moja, tukiharibu hii Kenya na vita, tuharibu mali yetu ," rais aliwaambia wananchi, " eti tukijenga barabara kama hii, wengine wanakuja kuweka mipira hapa wanachoma, inaharibika na tunalazimika kutafuta pesa ingine ya kutengeneza, Si hiyo ni upumbavu?"
Katika maandamano ya Jumatano wizara ya usalama na mambo ya ndani ilisema kuwa watu 300 walikamatwa na maofisa wa usalama.
Hata hivyo watu wanne wameripotiwa walikufa huku maafisa wa usalama walilaumiwa na wananchi na amashirika kadhaa kwa kutumia nguvu.
"Sisi ni nchi ya demokrasia , sisi ni nchi ya amani," ameongeza.
Wito wa maongezi
Huku mvutano kati ya Serikali ya rais William Ruto na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga ukiendelea kumekuwa na wito kutoka kwa nchi na mashirika ya kimataifa ili watatue tatizo kwa njia ya maongezi.
Sasa msemaji wa muungano wa upinzani ,Azimio , Makau Mutua amesema kuna haja ya serikali kufanya maongezi ya amani.
" Serikali haiwezi kupigana kwa mafanikio na makasisi, nchi za Magharibi, Azimio, na wanaharakati kwa pamoja, "Makau Mutua amesema katika mtandao wake wa twitter, " njia pekee ya ni kukaa mezani kutafuta suluhu la kisiasa. Hufanyi amani na marafiki zako, bali na adui zako."
Lakini naibu wa rais Rigathi Gachagua amesema " serikali haiwezi kufanya maongezi na mhalifu".
Amedai kuwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga anatumia ujanja kutaka kuingia katika uongozi.
"Hakuna njia ya mkato ya uongozi ni moja, na hiyo ni kupitia kura," amesema akihutubia mkutano leo.
"Tunataka kuomba viongozi wetu wa kanisa, jamii ya kimataifa kwamba si sahihi kumuomba rais kuketi chini na mhalifu."
Anadai kiongozi wa upinzani ndiye chanzo cha watu kuuawa na mali ya watu kuharibiwa katika maandamano ambayo imefanyika.