Rais amesema mfumo huu utakuwa muhimu katika kupambana na uhalifu nchini Uganda. / Picha: AP

Rais Yoweri Museveni amesisitiza kuwa mradi wa usajili wa kidijitali wa nambari za gari za kidijitali lazima uendelee jinsi ulivyopangwa.

Mfumo huu, ulioundwa kufuatilia magari yote, pikipiki, na vyombo vingine vya usafiri katika eneo la mamlaka ya Uganda, unahitaji kifaa cha kielektroniki kubandikwa kwa kila gari.

Rais amesema mfumo huu utakuwa muhimu katika kupambana na uhalifu nchini Uganda.

"Sasa, nasisitiza suala la nambari za usajili za kielektroniki, litakuwa pigo kubwa sana kwa uhalifu kwa sababu watu wengi wanafanya uhalifu kwa kutumia gari au bodaboda (pikipiki), " alisema rais Museveni siku ya Jumatatu,

Maneno ya rais yanakuja huku wizara ya mambo ya ndani ikisema haijui ni nani alitia saini mkataba na kampuni ya Urusi ambayo inafaa kutimiza mradi huo.

"Sijawahi kusaini hiyo kitu, nikitia saini nachukua jukumu ikiwa sitawajibiki, sijui ni nani aliyesaini mambo haya yalioanza mwaka wa 2019," waziri wa mambo ya ndani Kahinda Otafire aliambia kamati ya bunge

Kandarasi hiyo ilitolewa kwa kampuni ya Urusi, Joint Stock Company Global Security, mwaka wa 2019, kutengeneza nambari kidijitali za magari yenye lengo la kuimarisha usalama nchini.

Mfumo huo ukaitwa “Intelligent Transport Management System” (ITMS).

Kampuni hii ingefaa kuendesha operesheni hii kwa miaka 10 kabla ya kuikabidhi kwa serikali ya Uganda.

Wamiliki wapya wa magari na pikipiki watalipa dola 192 kupata nambari za kidijitali huku wale ambao wamesajiliwa watalazimika kulipa dola 40 kwa magari na dola 13 kwa pikipiki, kubadilisha nambari zao.

Wananchi wengine nchini Uganda wanakubali kuwa ni mfumo mzuri wa kupambana na uhalifu, huku wengien wakisema kuwa ada inayotozwa kwa kupata nambari mpya ya kidijitali ni ya juu sana.

Kenya tayari imeanza

Mwezi Agosti mwaka 2022 Kenya ilizindua nambari za kizazi kipya kwa magari yote yanayoagizwa kutoka nje ya nchi , seriklai ikisema hii kwa nia ya kuzuia ukwepaji kodi na wizi.

Nambari hizi mpya za Kenya, ambayo zinatambulika kwa urahisi kwa maafisa wa kutekeleza sheria, pia zinahifadhi taarifa kama vile mwaka wa utengenezaji, aina na rangi ya gari, nambari ya injini, tarehe na mahali pa kutengenezwa, na maelezo ya bima.

Bado juhudi za watu kubadilisha nambari zao ili kuchukua hizi mpya za kidijitali zinaendelea.

TRT Afrika