Moses Kabali alikamatwa Septemba 3, 2024, na upekuzi katika makazi yake ulipelekea kupatikana kwa simu mbili za mkononi, laptop mbili na nyaraka mbalimbali. Picha: Kenya DCI

Kenya imemhukumu raia wa Uganda kifungo cha miaka mitano jela kwa mashtaka ya udanganyifu.

Kitengo cha makosa ya jinai Kenya, DCI kinasema ilibainika kuwa mnamo Juni 30, 2024, Moses Kabali alituma barua pepe kwa Sekretarieti Kuu ya Interpol nchini Ufaransa, akiwaomba watoe taarifa kwa vyombo vya usalama vya Kenya, haswa Kitengo cha Polisi cha Kupambana na Ugaidi (ATPU), kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio la kigaidi.

Aidha alidai kuwa watu wawili anaowafahamu wanaofanya kazi na magaidi wengine wasiojulikana walikuwa wakipanga kutekeleza shambulizi la kigaidi nchini Kenya kwa kutumia vilipuzi.

Wapelelezi wa ATPU walianzisha uchunguzi ambapo walimkamata mshukiwa wa kike ambaye nambari yake ya simu ilitajwa katika ripoti ya Kabali.

Alipohojiwa, alifichua kuwa nambari ya simu iliyotajwa ilikuwa imesajiliwa kwa kitambulisho chake lakini ilikuwa ikitumiwa na binamu yake.

Msako wa kumtafuta aliyetajwa ulianza, na alikamatwa huko Eastleigh, mtaa wa Jam, jijini Nairobi Agosti 31, 2024. Hata hivyo, uchunguzi zaidi ulifichua kwamba hakuwa na uhusiano na kundi lolote la kigaidi na hakujua kuhusu shambulio lolote lililopangwa.

Moses Kabali alikamatwa Septemba 3, 2024, na upekuzi katika makazi yake ulipelekea kupatikana kwa simu mbili za mkononi, laptop mbili na nyaraka mbalimbali.

DCI inasema uchunguzi wa kitaalamu katika Maabara ya Uchunguzi wa Kupambana na Ugaidi ulibaini kuwa Kabali ndiye mwandishi wa barua pepe hiyo kwani ilibainika kuwa barua pepe hiyo ilitoka kwenye akaunti yake ya barua pepe ya yahoo.

Kabali alifikishwa mahakamani na kuhukumiwa faini ya Sh5,000,000 au kutumikia kifungo cha miaka 5 jela.

TRT Afrika