Maafisa wa upelelezi nchini Kenya waliokuwa wanafuatilia kesi ya ulaghai mkubwa wa dhahabu ulioripotiwa nchini humo leo wamemfikisha mahakamani raia wa Marekani aliyehusishwa na kashfa iliyohusisha maelfu ya kilo za dhahabu iliyogharimu zaidi ya dola milioni 1.35.
Antonucci Sergio Patrick alifikishwa katika Mahakama ya Milimani akikabiliwa na shtaka la kula njama ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kufuatia kukamatwa kwake Disemba 15, 2024 baada ya kuingia nchini kutoka Dubai.
Uthibitisho uliofanywa baada ya uchunguzi wa kina unaonyesha kuwa Sergio alikutana na mlalamikaji mnamo Julai 2023 huko Nevada, Las Vegas, Marekani.
Sergio alijitambulisha kama mwekezaji wa zamani wa benki na mshauri wa kisheria aliyebobea katika kufanya biashara katika masoko ambayo yanachukuliwa kuwa magumu au tata na Marekani.
Akifurahishwa na maelezo hayo mlalamikaji alimpa kandarasi Sergio, kulinda shughuli zake za dhahabu barani Afrika akidhani kuwa alikuwa na leseni na kumlipa bonasi ya Dola 50,000 mnamo tarehe 29 Agosti, 2023.
Hii ilifuatiwa na na Malipo ya Dola za Marekani 15,000 tarehe 24 Januari, 2024 na Dola za Marekani 15,000 zaidi tarehe 28 Februari 2024.
Katika mpango huo ambao pia umeshuhudia mshirika wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eric Kalala Mukendi akishtakiwa, mlalamikaji alilazimishwa kusafiri hadi Nairobi ambapo Sergio alimtambulisha kwa mshirika mwengine wa Kimarekani, Caden Gebhard, ambaye aliwasilishwa kama afisa wa usalama wa Marekani wa kikundi cha vikosi maalum.
Inadaiwa, Caden alikuwa muhimu katika biashara hiyo kwani alikuwa na mawasiliano katika eneo hilo.
Ni kufuatia mkutano huo ambapo mlalamishi pia alitambulishwa kwa anayedaiwa kuwa mmiliki wa dhahabu hiyo na msafirishaji aliyeidhinishwa. Mkutano ulifanyika katika Hoteli ya Four Points Sheraton huko Hurligham, Nairobi.
Bila kujua kuna njama ya kumfilisi muathiriwa kupitia kampuni yake ya AURUMSIC ONE LLC aliingia Mkataba wa mauzo na ununuzi na kampuni ya muuzaji kwa jina la AERO Logistics.
Mkataba ulihusisha mauzo ya dhahabu ya kilo 2,820 ambapo aliishia kulipa kiasi cha dola 1,271,200 katika shughuli hiyo iliyofanyika tarehe tofauti kati ya 31 Machi, 2024 na 30 Mei, 2024.
Mwishowe, hakuna shehena iliyowasilishwa na kusababisha muathiriwa kuripoti polisi.
Antonucci Sergio Patrick alifikishwa mahakamani.
Alikana mashtaka na akapewa bondi ya dola 77,500 ( Sh10 milioni ) pamoja na kutakiwa kuwa na mdhamini mmoja wa Kenya.
Januari 23, 2025 mahakama itataja siku ya kusikilizwa kwa kesi hiyo.