KWS inasema mamake pundamilia alikabiliwa na matatizo baada ya kujifungua/ Picha : KWS

Maafisa wa wanyamapori wamemuokoa pundamilia aliyekutwa akinyonya mzoga wa mama yake kaskazini mwa Kenya.

Kwa mujibu wa Shirika la Wanyapori la Kenya(KWS) mama Pundamilia huyo alikufa baada ya kupata tatizo wakati wa kuzaa.

Kwa sasa, pundamilia huyo mdogo, jamii ya Grevy's ambao wanatajwa kuwa hatarini kutoweka, kulingana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Asili(IUCN) amehamishiwa katika kituo cha uokoaji na kulea wanyama, ingawa siku yake ya kuzaliwa bado haijafahamika.

"Uokoaji huu uliofanikiwa sio tu uliokoa pundamilia, pia uliweka msisitizo kwenye umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori," imesema KWS.

Mtoto huyo wa pundamilia amehamishiwa katika kituo cha uokoaji wanyama/ Picha kutoka KWS 

Idadi ya pundamilia aina ya Grevy porini inakadiriwa kuwa takriban 2,800 na wengi wanapatikana kusini mwa Ethiopia na kaskazini mwa Kenya, kulingana na Shirika la Wanyamapori la African Wildlife Foundation(AWF).

Kupitia tovuti yake, AWF inasema kuwa watoto wa wanyama hawa hutegemea maziwa ya mama zao hadi wanapofikisha umri wa miezi sita hadi nane.

TRT Afrika