Spika wa Bunge la Uganda Rebecca Among akiwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni / Picha: Ikulu Uganda

Spika wa Bunge la Uganda Rebecca Among amesema kuwa Rais Museveni aliamuru ripoti ya ukaguzi wa kisayansi kuhusu wizi wa fedha wa zaidi ya dola milioni 17 katika Benki Kuu ya Uganda kukabidhiwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ya Polisi kwa ajili ya usimamizi zaidi.

Amesema hii ni kutokana na ushahidi wa hatia ulioibuliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika shughuli hiyo ya kashfa.

Novemba 2024 serikali ya Uganda ilikiri kwamba akaunti za Benki Kuu ya nchi hiyo zilidukuliwa na zaidi ya dola milioni 17 kuibiwa.

“Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amefanya kazi nzuri sana, wamefanya uchunguzi wa kitaalamu na wamenipa ripoti, ripoti ipo. Nimekuwa nikishauriana na Rais juu ya jambo hili na kuona kuwa vitu vilivyopatikana hapo ni vya uhalifu," Among aliliambia Bunge.

"Kwa sababu ya uhalifu huo, tungeelekeza ripoti hii ipelekwe moja kwa moja kwenye Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID) kwa usimamizi zaidi. Na CID watatuletea taarifa kuhusu hatua iliyochukuliwa,” Spika Among aliongezea.

Hata hivyo, sehemu ya wabunge wamepinga uamuzi huo wakiongozwa na Geoffrey Ekanya Mbunge wa Tororo Kaskazini na Wilfred Niwagaba Mbunge wa Ndorwa Mashariki, wote hao walipinga uamuzi wa Spika na Rais Museveni kukabidhi ripoti ya Benki ya Uganda moja kwa moja kwa Polisi, badala ya kuchunguzwa na vyombo husika.

"Kanuni zinakupa mamlaka na wewe ni Mwenyekiti wa Kamati zilizoainishwa kushughulikia jambo lolote ambalo ni la jinai na usalama," Geoffrey Ekanya Mbunge wa Tororo Kaskazini amesema.

"Sijapendezwa na ripoti ambayo imetolewa kuhusu Benki ya Uganda lakini ningefikiri kwamba kwa kutumia uwezo wako ripoti hiyo ingeshughulikiwa na Kamati unayoiongoza, hiyo ni Kamati ya Maadili kabla ya kupelekwa kwengine ,” alibaini Ekanya.

“Nilidhani hii ni ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ambayo kwa kawaida ripoti hiyo ingepitishwa kwa Kamati ya Bunge hili ambayo ingeamua ni ripoti gani ingejadiliwa na Bunge hili na kamati ipi ingeamua kupeleka ripoti kuu ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kwa mamlaka husika ya uchunguzi,” aliteta Wilfred Niwagaba , Mbunge wa Ndorwa Mashariki.

Novemba 2024 Waziri wa Fedha wa nchi alisisitiza kuwa ataleta tena ripoti Bungeni baada ya uchunguzi kukamilika.

TRT Afrika