Polisi Kenya wamepiga marufuku maandamano jijini Nairobi

Polisi Kenya wamepiga marufuku maandamano jijini Nairobi

Polisi wanasema magenge ya wahalifu yameingilia maandamano dhidi ya serikali.
Maandamano yanayohusisha hasa vijana yalianza Kenya Juni 2024 / Picha: Reuters

Polisi wa Kenya wamepiga marufuku maandamano katikati mwa mji mkuu, Nairobi, hadi ilani nyengine kufuatia wiki kadhaa za maandamano ya kuipinga serikali ambayo walisema yamepenyezwa na magenge ya uhalifu yaliyopangwa.

Baadhi ya wanaharakati waliwataka watu kukusanyika siku ya Alhamisi wakiwa na vifaa vya kupigia kambi katika bustani ya Uhuru iliyo karibu na eneo la biashara la mji, huku kukiwa na msururu wa polisi kote Nairobi.

Takriban watu 50 wameuawa katika maandamano yaliyoongozwa na vijana kupinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru yaliyozuka kote nchini Kenya mwezi mmoja uliopita na yameendelea hata baada ya Rais William Ruto kuondoa muswada huo na kutimua baraza lake lote la mawaziri.

Wanaharakati wanasema kuwa wanataka Ruto ajiuzulu na wanataka mageuzi yafanyike ili kusafisha ufisadi na kushughulikia utawala duni.

Kuingiliwa na wahalifu

"Tuna taarifa za kijasusi zinazoaminika kwamba makundi ya wahalifu waliopangwa yanapanga kuchukua fursa ya maandamano yanayoendelea kufanya uhalifu, ikiwa ni pamoja na uporaji," Mkuu wa Polisi Douglas Kanja Kiricho alisema katika taarifa Jumatano jioni.

"Hakuna maandamano yatakayoruhusiwa katika Wilaya ya Biashara ya Kati ya Nairobi na mazingira yake hadi ilani nyengine ili kuhakikisha usalama wa umma."

Maandamano hayo ambayo yameandaliwa mtandaoni bila kuungwa mkono na wanasiasa wa upinzani, yamezua mzozo mkubwa zaidi wa miaka miwili ya Ruto mamlakani.

Katika makubaliano yake ya hivi punde kwa madai ya waandamanaji, Ruto wiki jana aliahidi kuunda serikali yenye msingi mpana, lakini muungano wa upinzani Jumatano ulikataa wazo hilo, ukitaka kuitishwa kwa kongamano la katiba.

Bunge lilivamiwa

Maandamano hayo yalianza kwa amani lakini baadaye iligeuka kuwa ya vurugu. Baadhi ya waandamanaji walivamia bunge kwa muda mfupi Juni 25, na polisi walifyatua risasi.

Ofisi ya Ruto ilipanga mazungumzo ya "sekta mbalimbali" wiki hii ili kushughulikia malalamiko ya waandamanaji, lakini kufikia Alhamisi hapakuwa na dalili zozote kuwa walikuwa wameanza.

Viongozi wengi walioongoza maandamano hayo wamekataa mualiko huo, badala yake wametaka hatua za haraka zichukuliwe kuhusu masuala kama vile rushwa.

"Polisi na Rais Ruto hawana uwezo wa kusimamisha haki zilizohakikishwa na katiba," mwanaharakati Boniface Mwangi aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X akijibu marufuku ya maandamano.

Vyombo vya habari vimetahadharisha

Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA), imevionya vyombo vya habari dhidi ya "kuendeleza" ghasia katika uandishi wao wa maandamano, "ambayo yanaweza kusababisha machafuko makubwa ya wenyewe kwa wenyewe nchini."

Mkuu wa CA David Mugonyi amesema baadhi ya vyombo vya habari vimekosa kutoa ripoti zinazozingatia usawa, aliandika katika barua ya Julai 17 kwa mtendaji mkuu wa vyombo vya habari iliyoonekana na Reuters.

TRT Afrika