Polisi nchini Ghana wanawasaka washukiwa baada ya sanamu ya Rais anayemaliza muda wake, Nana Akufo-Addo, kuharibiwa katika Mkoa wa Magharibi mwa nchi hiyo.
Mnara huo wa ukumbusho uliharibiwa kwenye upande wa kushoto, Polisi imesema katika taarifa.
"Juhudi za polisi zinaendelea za kuwakamata wahusika ili wakabiliwe na haki," ilisema.
Rais Akufo-Addo alikabiliwa na msukosuko baada ya kuzindua sanamu hiyo mwezi Novemba 2024 kusherehekea kukamilika kwa ahadi alizotoa kabla ya kuingia madarakani.
Alikashifiwa kwa kujitukuza na baadhi ya wakazi katika eneo hilo na wengine waliripotiwa kutishia kuliondoa pindi atakapoondoka madarakani.
Sanamu hiyo iliharibiwa Jumatatu asubuhi, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya Ghana.
Rais Akufo Addo atamaliza muda wake Januari 2025 baada ya mihula miwili ya kuwa madarakani.
Mgombea wa upinzani na Rais wa zamani John Mahama alishinda uchaguzi wa urais mapema mwezi huu kwa takriban asilimia 57 ya kura ikiwa idadi kubwa ya ushindi katika zaidi ya miongo miwili.
Mahama anatazamiwa kuapishwa tarehe Januari 7, 2025 na ameahidi mwelekeo mpya wa nchi.