Idara ya uhamiaji nchini Kenya imetangaza kuwa itaanza kuchapisha hati ya kusafiria, pasipoti usiku na mchana kila siku kwa ajili ya kutoa huduma hii kwa wananchi.
Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani alisema kuwa kuna takriban pasipoti 58,000 ambazo hazijachapishwa, akidai kuwa kuna ufisadi katika idara ya uhamiaji inayoshughulikia pasipoti.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Evelyn Chelugut alitangaza Jumatatu kuwa hii ni kwa ajili ya kukabiliana na mrundikano wa pasipoti ambazo watu wamengojea kwa miezi , na wengine zaidi ya mwaka mmoja.
Amesema zamu za operesheni hii mpya zitaendelea kwa saa 14 na maombi yatapokelewa kuanzia saa 1 asubuhi hadi 3 usiku.
Alisema pia mipango inaendelea ya kununua vifaa vipya vya kuchapisha pasipoti kwa saa 24.
Kuna watu ambao wamengoja pasipoti zao kwa zaidi ya mwaka mzima, huku wengine wakisema walilazimika kutoa hongo ili kupata pasipoti zao.