Seneta wa Makueni nchini Kenya, Dan Maanzo amewasilisha ombi la kumshutumu Rais William Ruto kwa kile anachodai mwenendo wa kutiliwa shaka akiwa madarakani.
Maanzo anahoji kuwa Ruto amekiuka Katiba katika masuala mengi, ikiwa ni pamoja na kushindwa kuwalinda Wakenya dhidi ya ukatili wa polisi kwa mujibu wa vipengee vya 131 na 25 vya Katiba kuhusu haki za kimsingi na uhuru wa Wakenya, pamoja na kukuza na kuimarisha umoja wa taifa.
Seneta huyo aliteta zaidi kuwa Ruto amewatenga baadhi ya Wakenya na kuendelea kuzidisha mivutano katika taifa kwa kukosa kuhakikisha kuna ushirikishwaji mwafaka wa umma katika utekelezaji wa siasa zake.
Katia ya miradi ambayo ametoa mfano ni Hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF), muundo wa ufadhili wa Chuo Kikuu, Ushuru wa Nyumba, kashfa ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) inayohusishwa na kampuni ya Adani Holdings miongoni mwa zingine.
Kwa hivyo Maanzo aliomba Seneti imchunguze Rais na mienendo yake ikaguliwe.
Ombi lake linakuja huku tayari kuna muswada bungeni wa kutaka kumuondoa naibu wa rais Rigathi Gachagua kwa madai kuwa amekiuka sheria tofauti za nchi.