Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua alichaguliwa kwa pamoja na Rais William Ruto katika uchaguzi wa Agosti 9, 2022. / Picha: Reuters

Na Brian Okoth

Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua, ambaye anakabiliwa na uwezekano wa kushtakiwa na kuondolewa madarakani, amesema atajitetea mbele ya Bunge la Kitaifa la nchi hiyo siku ya Jumanne.

Gachagua, ambaye alihutubia taifa kutoka katika makazi yake rasmi katika mji mkuu Nairobi siku ya Jumatatu, alisema atafika bungeni ili kujitetea.

Bunge la Kitaifa, lenye wajumbe 349, litasikiliza utetezi wa Gachagua na baadaye kupiga kura ya kumshtaki au la.

Angalau thuluthi mbili ya wanachama - sawa na 233 - wanahitaji kupiga kura kuunga mkono kushtakiwa kwake, ili uamuzi huo upelekwe kwa Seneti.

'Upataji wa mali haramu'

Bunge la Seneti lenye wabunge 67 pia litasikiliza mashtaka hayo, na ikiwa zaidi ya theluthi mbili - au wabunge 45 - watapiga kura kumshtaki Gachagua, naibu rais atalazimika kuondoka ofisi yake.

Miongoni mwa sababu nyingine, Gachagua anatuhumiwa kujipatia utajiri wa thamani ya shilingi bilioni 5.2 za Kenya, au dola milioni 40.3 za Marekani, kinyume cha sheria katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mwengi Mutuse, mwasilishaji wa hoja ya kumtimua Gachagua, anasema katika miaka miwili iliyopita, naibu wa rais alipokea mshahara wa shilingi milioni 24, au dola 186,000 za Marekani.

Mutuse aliongeza kuwa katika maandalizi ya uchaguzi wa urais wa Agosti 2022, Gachagua alitangaza utajiri wake kuwa shilingi milioni 800, au dola milioni 6.8 za Marekani.

'Kuidharau serikali'

Naibu Rais Gachagua, 59, pia anadaiwa kuhujumu serikali, na pia kujihusisha na siasa za kikabila.

Amekuwa akizungumzia masilahi ya jamii ya Kenya ya Kati yenye utajiri wa kura, anakotoka.

Kwa hivyo, amekabiliwa na shutuma za kuangalia ustawi wa sehemu moja pekee ya Kenya, badala ya kuakisi kanuni za afisi yake kama kiongozi wa kitaifa.

Gachagua alisema Jumatatu kwamba anatarajia wabunge watamsikiliza " siku ya Jumanne, wakati atakapo jitetea.

Zoezi baya la ushiriki wa umma

Naibu rais, ambaye alitaja madai dhidi yake kama "uongo wa kustaajabisha", alisema zaidi timu yake ya mawakili itawasilisha ombi mahakamani, kupinga jinsi ushiriki wa umma katika pendekezo la kuondolewa kwake ulivyoendeshwa wiki iliyopita.

Akielezea ushiriki wa umma kama "mbaya", Gachagua alisema zoezi hilo "halikidhi kiwango cha kikatiba."

Naibu rais wa Kenya alizidi kutetea biashara zake, ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na hoteli, kuwa ni halali, akisema ana ushahidi jinsi alivyopata biashara hiyo.

Aliongeza kuwa baadhi ya mali yake alirithi kutoka kwa nduguye marehemu Nderitu Gachagua, ambaye alikuwa mfanyabiashara na gavana wa kaunti ya Nyeri ya Kati mwa Kenya.

Baadhi ya watu walitarajia Gachagua kutangaza kujiuzulu Jumatatu, lakini naibu wa rais anasema yuko tayari kupigana, ikiwa ni pamoja na kujitetea mahakamani, kuthibitisha kutokuwa na hatia.

TRT Afrika