Madini tofauti ikiwemo dhahabu huchimbwa kwenye eneo hilo./Picha: Reuters

Hofu na hali ya kukata tamaa inazidi kuongezeka huku jitihada za kuwaokoa wachimba migodi 20 walionaswa nchini Nigeria, kufuatia kuporomoka kwa mgodi.

Mtu mmoja anahofiwa kufa na wengine sita waliokolewa wakiwa na majeraha makubwa baada mgodi huo kuporomoka siku ya Jumatatu, kufuatia kunyesha kwa mvua kubwa katika eneo hilo, maofisa wamesema.

Ibrahim Audu Husseini, msemaji wa taasisi ya kutoa msaada ya SEMA iliyoko katikati ya Jimbo la Niger, aliambia AFP siku ya Ijumaa kuwa zoezi la uokoaji lilizidi kuwa "gumu tofauti na ilivyotarajiwa".

Alisema kuwa waokoaji hao walilazimika kutumia patasi na nyundo ili kuwafikia wachimbaji walionaswa kutokana na kukosekana kwa vitendea kazi katika eneo hilo ambalo lipo katika wilaya ya mbali inayokabiliwa na magenge yenye silaha kali.

Hofu kubwa

Husseini alisema kuwa kulikuwepo na dalili kuwa wachimbaji hao walikuwa wamekufa.

"Harufu ya maji yanayotoka kwenye shimo imezidi kuwa kali na kuibua hofu kubwa," alisema.

"Hatuwezi kuhitimisha kuwa wachimbaji walionaswa wamekufa kwa sababu hakuna maiti iliyopatikana lakini harufu mbaya kutoka kwa maji kwenye shimo inatupa ishara ya wazi."

Idadi kamili ya wachimbaji madini walionaswa bado haijafahamika huku maafisa wakitoa maelezo yanayokinzana.

Siku ya Jumatano, taasisi hiyo ilisema kuwa idadi hiyo ilikuwa zaidi ya 30, huku siku ya Alhamisi polisi wakiambia AFP mhandisi katika eneo hilo "alithibitisha kuwa watu 20 wamenaswa", na kuongeza kuwa uchunguzi ulikuwa umeanzishwa.

Vifaa duni

Msemaji wa SEMA Husseini aliongeza kuwa "serikali haina vyovyote vya kuchimbia."

Alieleza kuwa mawe yaliporomoka na kufunika mgodi wakati wa mvua kubwa.

Wafanyakazi kwa kawaida hutumia baruti kuvunja mwamba huo, alisema, lakini wamekataza hilo kwani walichukua "tahadhari kubwa ili wasihatarishe maisha ya wale walionaswa".

"Ni zoezi la kuchosha lenye kuhitaji uvumilivu," alisema.

Madini tofauti kama vile dhahabu, tantalite na lithiamu huchimbwa katika eneo hilo.

Matukio ya unyang'anyi

Shiroro ni mojawapo ya wilaya kadhaa katika Jimbo la Niger zinazotishwa na majambazi, ambao huvamia vijiji vya mbali kaskazini-magharibi na katikati mwa Nigeria ili kupora na kuteka watu nyara.

Kulingana na SEMA, watu sita walitekwa nyara katika eneo hilo siku ya Jumapili na wengine 20 kutekwa nyara karibu na eneo hilo hilo siku ya Jumanne.

Mwaka jana, serikali ya Jimbo la Niger ilipiga marufuku shughuli za uchimbaji madini huko Shiroro na wilaya zingine kutokana na ukosefu wa usalama.

Hata hivyo, wachambaji wadogo wameendelea kufanya kazi, kwa nia ya kujipatia pesa kwa ajili ya chakula na mahitaji muhimu baada ya uvamizi wa majambazi kuwafukuza wengi kutoka kwa nyumba na mashamba yao.

TRT Afrika