Uondoaji wa wanajeshi wa Marekani kutoka Niger umekamilika, afisa wa Marekani alisema Jumatatu.
Idadi ndogo ya wanajeshi waliopewa jukumu la kulinda Ubalozi wa Marekani wamesalia, msemaji wa Pentagon Sabrina Singh aliwaambia waandishi wa habari.
Mapema mwaka huu, utawala wa kijeshi wa Niger ulihitimisha makubaliano yaliyoruhusu wanajeshi wa Marekani kufanya kazi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Miezi michache baadaye, maafisa kutoka nchi zote mbili walisema katika taarifa ya pamoja kwamba wanajeshi wa Marekani watamaliza kuondoka katikati ya Septemba.
Kambi ya mwisho ya kijeshi
Marekani ilikabidhi kambi zake za mwisho za kijeshi nchini Niger kwa mamlaka za mitaa mwezi uliopita, lakini takriban wanajeshi 22 wa Kimarekani walikuwa wamebaki Niger, hasa kwa ajili ya majukumu ya kiutawala yanayohusiana na uondoaji huo, Singh alisema.
Kuondolewa kwa Niger kwa wanajeshi wa Marekani kufuatia mapinduzi ya mwaka jana kuna madhara makubwa kwa Washington kwa sababu inawalazimu wanajeshi kuacha kambi muhimu ambazo zilitumika kwa misheni ya kukabiliana na ugaidi huko Sahel.
Vikundi vya waasi vinafanya kazi katika eneo kubwa kusini mwa jangwa la Sahara. Mojawapo ya makundi hayo, JNIM, inafanya kazi nchini Mali, Burkina Faso na Niger, na inatazamia kupanuka hadi Benin na Togo.
Wanajeshi wa Ufaransa pia waliondolewa
Niger ilikuwa imeonekana kuwa mojawapo ya mataifa ya mwisho katika eneo hilo lenye machafuko ambayo mataifa ya Magharibi yangeweza kushirikiana nayo ili kukomesha uasi unaokua wa wanamgambo.
Marekani na Ufaransa zilikuwa na wanajeshi zaidi ya 2,500 katika eneo hilo hadi hivi karibuni, na pamoja na nchi nyingine za Ulaya zimewekeza mamia ya mamilioni ya dola katika usaidizi wa kijeshi na mafunzo.
Katika miezi ya hivi karibuni Niger imejiondoa kutoka kwa washirika wake wa Magharibi, na badala yake kugeukia Urusi kwa usalama.
Mnamo Aprili, wakufunzi wa kijeshi wa Urusi walifika Niger ili kuimarisha ulinzi wa anga wa nchi hiyo.