Ufaransa ilitua ndege ya kijeshi nchini Niger siku ya Alhamisi asubuhi licha ya kufungwa kwa anga baada ya kutangazwa kwa mapinduzi Jumatano usiku, Kanali wa jeshi Amadou Abdramane alisema kwenye televisheni ya taifa.
Wizara ya mambo ya nje na ulinzi ya Ufaransa pamoja na jeshi la Ufaransa hawakujibu mara moja maombi ya maoni, shirika la habari la Reuters linaripoti.
Jeshi kuungana
Mapema leo Mkuu wa jeshi la Niger alitangaza kusaidia wanajeshi walio nyuma ya jaribio la mapinduzi
Mkuu wa vikosi vya jeshi la Niger ameelezea kuunga mkono wanajeshi walio tangaza kuwa wametwaa madaraka.
Kikundi cha wanajeshi kilichoandaa njama ya mapinduzi kinajiita "Vikosi vya Ulinzi na Usalama" (FDS), walitangaza kuwa wameamua "kumaliza utawala," na kutangaza kuwa taasisi zote zimesimamishwa, mipaka imefungwa, na amri ya kutotoka nje usiku imewekwa.
Wakati asasi za Kiafrika na kimataifa zikilaani kuchukua madaraka kwa nguvu na washirika Ufaransa na Marekani wakielezea uungwaji mkono kwa kiongozi wa kidemokrasia wa Niger, Mohamed Bazoum.
"Mkuu wa jeshi... ameamua kuidhinisha tangazo lililotolewa na Vikosi vya Ulinzi na Usalama... ili kuepuka mzozo wa mauti kati ya vikosi tofauti," alisema Mkuu wa vikosi vya jeshi, Jenerali Abdou Sidikou Issa, katika taarifa.
Waziri wa Mambo ya Nje ajitangaza kama kiongozi wa nchi kwa muda
Waziri wa mambo ya nje wa Niger Hassoumi Massoudou, amejitangaza kuwa kaimu waziri mkuu wa nchi hiyo huku wanajeshi wakiendelea kumshikilia rais wa nchi hiyo na kutangaza kuwa wamepindua serikali.
Kikundi cha wanajeshi kimetangaza kuwa kimemuondoa rais Mohamed Bazoum kutoka mamlakani .
Waziri huyo amesema katika mtandao wake wa X ( twitter) kuwa serikali iliyochaguliwa ndiyo "mamlaka halali na ya kisheria".
Waziri wa ulinzi anaripotiwa kuto kuonekana na inasemekana kuna uwezekano mkubwa amekamatwa.