Ubelgiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC zimeingia katika mzozo wa kidiplomasia baada ya mahakama mjini Kinshasa kuidhinisha hukumu ya kifo Jumatatu kwa mtaalamu wa masuala ya kijeshi mwenye uraia ya Ubelgiji na DRC.
Mahakama ya kijeshi ilitoa uamuzi huo kwa Jean-Jacques Wondo katika kesi ya rufaa kwa madai ya kupanga mapinduzi ya mwaka jana nchini DRC , wakili wake alisema Jumatatu.
Jumatatu, serikali ya Ubelgiji ilimuondoa balozi wake mjini Kinshasa mara moja kwa mashauriano na kumwita balozi wa DRC mjini Brussels "kuelezea kusikitishwa kwao," kulingana na taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje.
"Hukumu hii ya kifo kwa raia wetu haiwezi kuchukuliwa kirahisi... kutokana na udhaifu mkubwa wa vipengele vilivyowasilishwa wakati wa kesi na ukosefu wa ushahidi wa kumtia hatiani," iliongeza.
Wondo, mtaalam wa masuala ya kijeshi anayefanya kazi na idara ya ujasusi ya DRC, alikuwa mmoja wa watu 37 waliohukumiwa kifo kwa kile jeshi la DRC linasema kuhusika katika jaribio la mapinduzi lililokabiliwa Mei 2024.
Mfumo wa sheria wa kijeshi wa DRC unaamini kuwa Wondo ni kati ya waliopanga njama ambapo watu wenye silaha walishambulia nyumba ya waziri mmoja kabla ya kuelekea ofisi za Rais Felix Tshisekedi.
Wondo amesubiri kwa muda wa miezi minne na nusu baada ya hukumu yake ya awali ya mwezi Septemba 2024, na siku ya Jumatatu mahakama ya rufaa ikathibitisha hukumu hiyo ya kifo.
Mashirika kadhaa ya haki za binadamu yametaka hukumu za kifo zibadilishwe na kuwa kifungo cha maisha jela.
Hukumu za kifo pia zilitolewa kwa watu wawili wenye uraia pacha wa Uingereza na Canada pamoja na DRC kama Wondo, pamoja na raia watatu wa Marekani.
Mwezi Machi 2025, serikali ya DRC ilirejesha hukumu ya kifo ambayo ilikuwa imeanza kutumika tangu mwaka 2003.
Ilisema hii ilikuwa kuwalenga wanajeshi wanaohusishwa na uhaini.